Wizara ya Madini  imekutana na Wawekezaji Wakubwa na wa Kati wanaofanya shughuli za  uchimbaji wa madini  katika maeneo mbalimbali nchini.


Wadau hao wamekutana Februari 14, 2023 jijini Dar Es Salaam katika kikao kilicholenga kupokea maoni kuhusu Kanuni za Madini ( Ushiriki wa Serikali) za Mwaka 2022.


Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema  Wizara imeona ni vema kukutana na wadau hao ili kuboresha Kanuni hizo pale inapoona inafaa kwa kuwa tangu kuanza kutumika kwake Serikali imekua ikipokea maoni kutoka kwa wadau hao.


Ameongeza kwamba,  Serikali inashiriki  uwekezaji  huo  kwa  Mujibu wa  Kifungu  cha  10   cha Sheria ya Madini Sura 123 kinachoeleza ushiriki wa Serikali kwenye uwekezaji katika miradi  mikubwa ya madini.


" Ni suala  jema na haki ya wadau  kutoa maoni kwa sababu kuna njia kama mbili ambazo tunaweza kuzitumia kutunga  Kanuni.  Kuzitunga halafu ukawapa wadau wakatoa maoni au ukatunga kutokana na maoni yanayotolewa na wadau," amesema Dkt. Mwanga.


Ameongeza kwamba,  vikao kama hivi vitakua endelevu na pale itakapobidi kufanya marekebisho Serikali itafanya hivyo kulingana na hoja zinazotolewa.


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema  kikao hicho kimekuja kutokana na wizara kuendelea kupata maoni kutoka  Chemba ya Migodi   na kampuni moja moja.  Hivyo, Serikali imeona ni vema kukaa pamoja na wadau ili kuwezesha shughuli za migodi kufanyika vizuri baada ya kuboreshwa kwa Kanuni.


Mbali na wadau wa madini, kikao hicho pia kimehudhuriwa na watendaji na wataalam kutoka Wizara ya Madini  na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara.


Kwa upande wa wadau wameiomba Wizara kuendelea kukutana mara kwa mara na wadau ili kujadili changamoto zinazotokea katika utekelezaji wa Sheria kwa lengo la kuiwezesha Sekta ya Madini kukua na kuzidi kuchangia katika maendeleo na uchumi wa nchi.

Share To:

Post A Comment: