Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa ametoa maelekezo mahususi kwa baadhi ya maafisa misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wasio waaminifu katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam kujitafakari utendaji wao kabla ya kuwabaini na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mhe. Mchegerwa ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Ofisi ya TFS na kugawa pikipiki 43 ambazo zitatumika kwenye usimamizi wa raslimali za misitu hapa nchini. Ameambatana na Naibu Waziri wake Mary Masanja na Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi.

Aidha, amesisitiza kuwa baada ya kutoa vitendea kazi (pikipiki) hivyo Serikali itakwenda kuwapima utendaji kazi wao.

“Katika kipindi changu sitakubali kuwaacha watumishi wala rushwa, wabadhilifu na wanaotumia vibaya ya madaraka yao” amefafanua Mhe. Mchengerwa

Ameongeza kuwa angependa kuona mchango na utendaji wa kila mtendaji hasa baada ya kubadilika kwa taasisi hiyo kutoka kuwa taasisi ya kiraia na kutumia mfumo wa kijeshi.

Aidha, amesema tayari Makamu wa Rais, Mhe. Dkt, Philipo Mpango alishaagiza kusimamia uvunaji haramu wa misitu ikiwa ni pamoja na kukataa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa katika mkoa wa Pwani.

Amesisitiza kutangaza vivutio vya kiikolojia vya utalii vinavyotokana na uhifadhi wa misitu, kuandaa mpango wa ujenzi wa hoteli kwa ajili ya watalii wa ndani na nje.

Pia ameagiza kuongeza mkazo katika kutoa mafunzo mbalimbali kwa wananchi na ametaka aletewe mashauri yote ya kesi ili aweze kufuatilia na amefafanua kuwa anguko la kwenye mifumo ya usimaizi wa misitu ya Tanzania ni anguko la dunia.

Mwenyekiti wa Bodi wa ya TFS, Brigedia Mbarack Mkeremy amemshukuru Mhe. Waziri kwa maelekezo yake ambapo amemhakikishia kuwa wakala itakwenda kutekeleza mara moja.

Naye Katibu Mkuu mpya wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara imedhamiria kufanya kazi kwa kasi, umoja, ushirikiano na kuleta matokeo chanya kwenye usimamizi wa raslimali.

Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo amesema TFS inasimamia takribani misitu 463 kote nchini yanayojumuisha mashamba ya miti 24, Hifadhi za misitu ya mazingira asilia 20 na misitu ya mikoko katika mwambao wa bahari ya Hindi.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: