OR-TAMISEMI


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Angellah Kairuki ametoa maagizo 14 kwa Wahandisi wa Idara ya miundombinu na maendeleo ya vijijini na mijini kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Makatibu Tawala Wasaidizi sehemu ya miundombinu na Mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa Mikoa na Wilaya kutotoa kazi kwenye kampuni zao binafsi za ujenzi.


Kairuki ametoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Makatibu Tawala Wasaidizi Sekretariet za Mikoa(miundombinu), wakuu wa Idara za miundombinu na maendeleo ya vijijini na Mijini katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na mameneja wa TARURA Mkoa na Wilaya.


Amesema kumekuwepo na changamoto kadhaa ambazo zinaleta dosari katika utekelezaji wa majukumu yenu hivyo natoa maagizo haya Ili kuwa na ufanisi.


Kairuki amesema Kuna baadhi ya watendaji wana kampuni na ujenzi na maduka ya vifaa hivyo kuwataka kutojihusisha na kazi zinazotolewa na taasisi zao.


"Kwa wale wenye Kampuni msijihusishe na kazi  za ujenzi kwenye Taasisi zenu hata kama uko Wilaya X huruhusiwi kufanya kazi Wilaya Y, atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake."


Pia amewaagiza kutotoa kazi kwa upendeleo, kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuzi zake, kuwa na mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, kuandaa na kutunza takwimu ya kazi mnazosimamia na kuboresha mahusiano ya kikazi baina yao ili kuboresha utendaji kazi,


Aidha, Kairuki amewaagiza kusimamia kazi kwa mujibu wa Mikataba ili kuhakikisha ubora wa kazi unafikiwa, kazi inatekelezwa kwa gharama zilizopangwa, ubora wa kazi unazingatiwa na kazi zinakamilika kwa wakati.


Pia aliwataka kuhakikisha kuwa masharti ya mikataba yanatekelezwa na Makandarasi kuwasilisha dhamana zinazohitajika na  kuwakata liquidated damage pale wanapochelewesha kazi.


Wakati huo huo amewataka kufanya mapitio ya usanifu kwa kazi zinazofanywa na mhandisi mshauri na pale mapungufu yanapobainika kutoa taarifa TARURA Makao Makuu au Wizarani badala ya kukaa kimya na kuanza kulalamika kwa Mamlaka zisizo rasmi za kutatua changamoto hizo pia amewataka kufanya tathimini ya zabuni kwa weledi ili kupata makandarasi wenye sifa.


" Inapotokea mabadiliko ya kazi ombeni vibali, fedha zinapobaki zaidi ya asilimia 15 ombeni vibali hii ni kwa mujibu wa Mkataba wa Utekelezaji, hii ni kwa Wilaya, Mikoa na TARURA Makao Makuu, 


Mhe. Kairuki pia amewataka kuepuka upendeleo kwa baadhi ya watumishi, kwani unapompendelea mtumishi mmoja au wawili wengine wanaona, iwapo utendaji wa mtumishi hauridhishi mjulishe au mchukulie hatua;


" Toeni nafasi za mafunzo kwa usawa sio kila mara wanaokwenda ni wale wale, hii iwe katika ngazi zote, Makatibu Tawala Wasaidizi, Wakuu wa Idara,Wakurugenzi, Mameneja na Waratibu wa Miradi wapeni fursa wasaidizi wenu washiriki katika mafunzo yanapotokea isiwe kila mara ninyi pekee ndio mnashiriki."


Pia amemuagiza Mtendaji Mkuu TARURA kutoa maelekezo kwa Mameneja wa TARURA ngazi za Mikoa ili watoe taarifa kwa Wakurugenzi wa maeneo husika kuhusu Makandarasi waliopo ili Halmashauri ziweze kuwadai Kodi ya Huduma. 


" Ni vyema ukaangalia utaratibu wa uthibithisho wa malipo ya kodi ya huduma kabla ya kumlipa Malipo yanayofuata."


Awali, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Victor Seff amesema Wakala inatekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano ambao umelenga kufikia 85% ya barabara zinazohudumiwa na Wakala huo kupitika katika vipindi vyote vya mwaka na kuwa unatarajia kugharimu Sh trilioni 4.2

Share To:

Post A Comment: