Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda. 

Na Mashaka Kibaya, Tanga.

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania  (UWT) Taifa,  Mary  Chatanda amepongeza hatua ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kuondosha zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya Siasa akisema,imerejesha faraja kwa wananchi na wapenda amani.

Akiwa katika mkutano wake na wanahabari jana Jijini Tanga, Chatanda alisema, UWT inampongeza Dkt Samia kwa kufanya maamuzi yaliyoleta furaha isiyo na kifani kwa wananchi na wapenda amani.

Chatanda alisema kwamba, hatua hiyo imetoa majawabu kwa demokrasia ya nchi akitaja uondolewaji mikutano ya hadhara, kukwamua mchakato katiba mpya,kufanya marekebisho sheria mbalimbali ili kupanua wigo wa demokrasia.

"Maamuzi ya Rais Dkt Samia yameleta faraja kwa vyama vya siasa na hatawapenda amani wote, ameonesha uthabiti wa kauli zake kwa matendo"alisema Chatanda.

Aidha Chatanda amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kufanya mikutano yake bila lugha za matusi kwa maelezo kuwa ni muelekeo mpya wa nchi katika kuihami demokrasia.

"Mama Samia ni neema kutoka kwa Mungu matumaini mapya yamerejea katika kujenga demokrasia,UWT inaungana naye, kilio cha UWT ni kuona amani inatawala" alisema Chatanda.

Mwenyekiti huyo wa UWT amesisitiza umuhimu wa amani na utulivu kuendelea kutawala ili kutoa fursa kwa Rais Dkt Samia kuendelea kushughulika na kero za wananchi.

Amewataka viongozi wa UWT kufanya mikutano ya hadhara kwa kufuata taratibu zote akiwahimiza kusikiliza kero zote kwa lugha ya kistaarabu.

Katika mkutano huo pia Mary Pius Chatanda alitumia wasaa huo akiahidi kutoa shilingi Milioni moja kwa ajili ya kikundi cha hamasa kinachotoa mchango mkubwa kuhamasisha maendeleo.

Alisema amewiwa kutoa mchango wake huo baada ya wahamasishaji hao kuwa na mchango mkubwa kwa shughuli za chama na Serikali.

"Hata kipindi cha Mwalimu alikuwepo bibi Titi aliyekuwa akitangulia kwakuimba na kuzungumza kidogo halafu ndipo akawa anamkaribisha Nyerere"alisema Chatanda.

Chatanda amebainisha kuwa fedha hizo kwa kikundi hicho cha hamasazitawasaidia kujianzishia shughuli za kiuchumi na kuweza kujikwamua.

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: