Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo kulia na Mkurugenzi wa Utawala na menejimenti ya rasilimali watu wa Ruwasa Bwai Biseko kushoto, wakishuhudia maji yakitoka kwenye bomba baada ya uzinduzi wa mradi mpya wa maji katika kijiji cha Paradiso wilayani Mbinga.

 Na Muhidin Amri,Mbinga.


TATIZO la maji safi na salama lililokuwepo kwa muda mrefu kwa wakazi zaidi 1,893 wa kijiji cha Paradiso kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga,limemalizika baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho.

Mradi huo umegharimu Sh.milioni 249,877.23 fedha kutoka serikali kuu umetekelezwa na Ruwasa kwa kutumia mfumo wa force Account na umekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutoa huduma kwa wakazi wa kijiji hicho.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Clement Kivegalo aliyetembelea wilaya ya Mbinga kukagua utekelezaji wa miradi ya maji na kuzungumza na wananchi.

Sinkala alisema,kijiji cha Paradiso hakikuwa na huduma ya maji kwa muda mrefu kutokana na mradi uliokuwepo kuchakaa tangu miaka ya 1990 na mradi huo ni miongoni mwa miradi 12 iliyotekelezwa kwa fedha za lipa kwa matokeo(PforR) katika wilaya ya Mbinga.

Alisema,kukamilika kwa mradi huo kumepunguza adha kubwa ya uhaba wa maji kwa watu wa kijiji hicho na umesaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko na jamii kupata muda mrefu wa kufanya kazi nyingine za kujiongezea kipato.

Alisema,katika mradi huo maji yanakuja kwa njia ya msereleko kutoka chanzo hadi kwenye tenki dogo umbali wa km3 na baada ya hapo yanasukumwa kwa pampu hadi kwenye tenki kubwa umbali wa km I kwa kutumia njia mbili ambazo ni umeme wa nishati jua na umeme wa Rea.

Aidha alieleza kuwa,mradi huo ni miongoni mwa skimu zinazosimamiwa na chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii ya NAMRU-CBWSO katika kata mbili za Ruanda na Namswea ambazo zina wajibu wa kukusanya maduhuli kwa ufanisi.

Sinkala alibainisha kuwa,hadi kufikia mwezi Novemba mwaka jana tayari kaya 24 zimeunganishiwa maji na chombo kimekusanya zaidi ya Sh.milioni 17,495,800.00.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Clement Kivegalo,amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kamati za maji ili mradi huo uwe endelevu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye,na uendelee kuwa suluhisho ya shida ya maji ilikuwepo kwa muda mrefu.

Alisema,Ruwasa imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yote ya vijijini na kuhaidi ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote hapa nchini vitapata maji,na kuwataka wananchi kutunza vyanzo na kulinda miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

“nia ya serikali kupitia Ruwasa ni kumtua mama ndoo kichwani kwa kuhakikisha wananchi wa Paradiso na maeneo mengine hapa nchini wanapata huduma ya maji safi na salama, na lazima mtambue kuwa fedha zilizotumika kwenye mradi huu ni nyingi”alisema Kivegalo.

“pia naomba mradi huu usimamiwe kikamilifu ili wananchi wote waliokusudiwa kunufaika nao wapate maji wakati wote tena kwa gharama nafuu”alisema.

Aidha amemuagiza meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga, kuhakikisha anafikisha mtandao wa maji kwenye maeneo yote ili wananchi waweze kupata huduma ya maji kwa urahisi.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Agnes Mbilinyi,ameishukuru Ruwasa kwa niaba ya serikali kutekeleza mradi huo kwani umesaidia kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ambao tangu mwaka 1900 hawakuwa na huduma ya uhakika ya maji.


Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo kulia,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Paradiso kata ya Ruanda Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Agness Mbilinyi,baada ya kuzindua mradi mpya wa maji utakaowanufaisha wakazi wa kijiji cha hicho.

Tenki jipya lenye uwezo wa kuhifadhi lita 75,000 za maji lililojengwa na Ruwasa ambalo limeanza kuhudumia zaidi ya wakazi 1,893 wa kijiji cha Paradiso wilayani Mbinga.


Tenki la maji lililojengwa na serikali ya awamu ya kwanza mwaka 1983 katika kijiji cha Paradiso Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma ambalo kwa sasa halitumiki kutokana na uchakavu.
Share To:

Post A Comment: