Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi katika Shule ya Sekondari iliyojengwa kwa fedha za Serikali iliyopo katika Kijiji cha Ihanda, Kata ya Mlali inayotarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwaka huu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema na kulia ni Bw. Omary Nkullo.

SERIKALI imehimiza matumizi ya mbolea kwa wananchi wa Kijiji cha Mlali Iyegu kilichopo Kata ya Mlali katika Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma ili kuepuka upungufu wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa wingi kwa kutumia mbolea inayotolewa kama ruzuku kutoka Serikalini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokua akiongea na wananchi hao wakati wa ziara yake iliyolenga kusisitiza utunzaji wa mazingira, kilimo na kukahamasisha agenda ya elimu.

“Asilimia 90 ya Wakazi wa Kongwa ni wakulima na wanategemea kilimo kuendesha maisha yao. Nawasisitiza kufanya kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea kwani Serikali imeamua kuwapunguzia mzigo wa gharama kwa kuchangia asilimia 70 ya gharama hizo. Hakuna Serikali inayotaka kudhuru watu wake, mbolea inayotolewa ni bora na imepimwa kitaalamu. Hatutarajii kupata maombi ya chakula cha msaada kutoka Serikalini wakati uwezekano wa kutumia pembejeo bora na kupata chakula cha kutosha upo” Amesema Mhe Senyamule.

Katika ziara hiyo pia, Mhe. Senyamule aliweza kutembelea shule mpya ya Sekondari iliyojengwa kwa fedha za Serikali iliyopo katika Kijiji cha Ihanda, Kata ya Mlali inayotarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwaka huu. Shule hii inatarajiwa kuwa msaada kwa wanafunzi wa Kijiji hicho ambao walikua wakitembea umbali mrefu wa takribani kilometa 12 kila siku kwenda na kurudi.

“Nimefurahishwa na ukamilishwaji wa shule hii ambayo itaepusha watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule ya Sekondari Mlali. Serikali imetimiza wajibu wake hapa na wazazi mtimize wajibu wenu wa kuhakikisha watoto wanafika hapa shuleni” Amesisitiza Mhe Senyamule

Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Remidius Mwema, amesema kuwa walipokea fedha za ujenzi wa madarasa 70 katika Wilaya yake na yote yamekamilika hivyo watahakikisha watoto wote 7,719 wanaotarajiwa kuanza shule mwaka 2023, wanawasili shuleni. “Tumeweka jitihada za uandikishwaji wa shule za awali na msingi kwa kwa kuhimiza mabalozi na wenyeviti wa Mitaa kutembea nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mtoto anayestahili kwenda shule anakwenda”

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa Bw. White Zuberi amesisitiza suala la elimu kwa kusema; “Tumetumia fedha za Madarasa kujenga shule mbili ikiwemo hii ya Ihanda, Mhe. Rais anawasaidia watu wa chini kuweza kusoma mpaka ngazi ya juu kwa kutoa elimu bure kuanzia awali hadi kidato cha sita, hivyo tuunge mkono juhudi za Rais kwa kupeleka watoto shule”

Kwa upande wa sekta ya mazingira, Mhe. Senyamule ameendelea kuhimiza kampeni yake aliyoizindua Desemba 31 mwaka Jana kwa kuwataka wanakongwa kupanda miti ya kutosha na kutunza vyanzo vya maji pia kuepuka ukataji miti holela. Sambamba na hilo, alionyesha mfano kwa kupanda Miti kwenye eneo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na eneo la shule ya Sekondari Ihanda kama ishara ya kusisitiza wananchi kupanda miti na akasisitiza Wilaya hiyo kuhakikisha inafikia lengo la agizo la Serikali la kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kwa mwaka.

Vilevile katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alitembelea mradi wa ujenzi wa kituo mahiri cha nafaka kilichopo eneo la Mtanana ambacho kitakua na utaalamu wa kuzuia sumu kuvu kwenye mazao. Mradi huu upo chini ya Wizara ya Kilimo na unagharimu takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 19.

“Nimepata taarifa kituo hiki ni kikubwa Afrika Mashariki na kati, kitawezesha mazao yetu kuuzika kimataifa. Nimefarijika kusikia kuwa kituo hiki kitatoa mafunzo, hivyo naamini kitatoa darasa tosha. Naahidi sisi kama Mkoa, tutaendelea kusimamia mradi huu ili ukamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa” Amesema Mhe. Senyamule.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa Bw. Omary Nkullo, amesema kujengwa kwa kituo hiki ni kutokana na historia iliyotokea miaka mitano iliyopita ambapo Mkoa ulipata vifo vya watu na wanyama kutokana na kula sumu kuvu kwenye mazao hivyo Wizara iliandaa mpango wa kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi na eneo hili tulihamisha wananchi kwa fidia ya Shilingi Milioni 8 hadi 9 na hati ya umiliki ikakabidhiwa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki.Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mlali, Wilayani Kongwa. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ambae alitoa fursa ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo na kuzipatia ufumbuzi, mkutano huo umefanyika mwishoni mwa wiki.

  

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo mahiri cha usimamizi wa mazao na nafaka kilichopo katika Kata ya Mtanana, Wilaya ya Kongwa. Kituo hicho kitakua na utaalamu wa kuzuia sumu kuvu kwenye mazao na ujenzi wake unagharimu takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 19. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius MwemaShare To:

Post A Comment: