Articles by "MBOLEA"
Showing posts with label MBOLEA. Show all posts

 Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema imetumia Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wadau kuhusu majukumu yake, fursa zilizopo katika sekta ya mbolea pamoja na mnyororo wa thamani wa uagizaji, utengenezaji na usambazaji wa mbolea nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Julai 4, 2026, Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini wa TFRA, Joshua Ng’ondya, amesema mamlaka hiyo imefika kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, umuhimu wa upimaji wa udongo, pamoja na utaratibu wa kujisajili ili kunufaika na mpango wa mbolea za ruzuku.

Amesema kupitia maonesho hayo, wananchi na wafanyabiashara wanapata maelekezo ya namna ya kupata leseni za biashara, kusajili maeneo ya biashara na kuanzisha viwanda vya uzalishaji wa mbolea, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika biashara ya mbolea nchini.

Ng’ondya amesema TFRA ina jukumu la kudhibiti ubora wa mbolea za viwandani na mbolea hai zilizosajiliwa, pamoja na kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuingia sokoni na katika mpango wa ruzuku kwa wakulima.

Aidha, ameeleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kutengeneza, kusajili na kuingiza mbolea sokoni kwa kufuata taratibu zilizowekwa, ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea bora, salama na zenye tija katika kuongeza uzalishaji wa mazao.

Katika kuhakikisha wakulima wa tumbaku wanapata ruzuku za mbolea Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, amefanya ziara ya kikazi katika vituo viwili vinavyo hakiki taarifa hizo mkoani Tabora kujionea maendeleo ya zoezi hilo na kuhakikisha linakamilika kwa wakati.

Baada ya kutembelea vituo hivyo katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo na ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Bw. Laurent amesema kuwa, zoezi hilo limefikia hatua nzuri itakayowezesha kuanza kwa taratibu za malipo kwa wakulima wa Tumbaku nchini. 

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Laurent ameeleza kuwa, lengo la uhakiki ni kuhakikisha wakulima wote waliozalisha Tumbaku katika msimu wa mwaka 2023/2024 wanalipwa na fedha hizo zinamfikia mkulima anayestahili moja kwa moja kupitia akaunti yake.

Ameeleza kuwa, zoezi hili linafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo, TFRA, TCDC na vyama vikuu vya ushirika vilivyo chini ya shirikisho la TCJE.

Akizungumza na Mkurugenzi Laurent, Ndg. Innocent Nsena Katibu Tawala wa Wilaya ya Urambo alieleza kuwa, suala la ruzuku limekuwa kilio cha muda mrefu kutoka kwa wakulima na kwamba utekelezaji wa mpango huu utapunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima.

“Ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ombi la kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku, kwa kuwa zao hili awali halikuwa miongoni mwa mazao yanayopata ruzuku” alisema Ndg. Nsena.

Kwa upande mwingine, akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi la uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika WETCU, kiongozi wa timu hiyo, Ndg. Byaga Nzohumpa, alieleza kuwa, zoezi hilo limekamilika kwa asilimia 100 baada ya kuhakiki taarifa za vyama vya msingi 248 walivyokabidhiwa.

Naye Ndg. Godwin Mwalongo, kiongozi wa timu ya uhakiki katika ofisi za Chama Kikuu cha Ushirika Mirambo, amesema kuwa, kazi ya uhakiki imefikia hatua nzuri na inatarajiwa kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TCJE, Ndg. Seleman Abasi Maona, alieleza kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa zilizokabili zoezi hilo ni uandaaji hafifu wa takwimu za wakulima wa tumbaku kwa msimu wa kilimo wa 2023/2024, hasa kutokana na taarifa zisizo sahihi kutoka kwa wakulima.

Alisisitiza kuwa kama kungekuwepo mfumo madhubuti wa ukusanyaji taarifa kuanzia ngazi ya chini, changamoto hizo zingeweza kuepukwa na kuahidi kuboresha kwa ajili ya manufaa ya baadaye kwa wakulima.











Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, amezihimiza taasisi za kilimo nchini kubadili mbinu za utendaji kwa kuachana na mazoea na badala yake kuimarisha matumizi ya utaalamu katika kuwawezesha wakulima kuongeza tija na kuendesha kilimo cha biashara.

Dkt. Diallo alitoa wito huo tarehe 19 Februari 2025, katika siku ya pili ya ziara ya Bodi na Menejimenti ya TFRA walipotembelea taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI – Maruku), Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo (MATI – Maruku), na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI). Ziara hiyo inalenga kuelewa majukumu ya taasisi hizo na kuimarisha ushirikiano katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea miongoni mwa wakulima.

Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Diallo amesisitiza kuwa ili kufanikisha malengo ya serikali kupitia kauli mbiu ya Agenda 10/30: Kilimo ni Biashara, wataalamu wa kilimo wanapaswa kuongeza jitihada katika kutoa elimu na ushauri kwa wakulima ili kubadili mitazamo hasi kuhusu matumizi ya mbolea na kuchochea uzalishaji wenye tija kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, ameeleza kuwa, ziara hiyo imetoa fursa kwa TFRA kufahamu kwa undani zaidi shughuli za taasisi hizo na kutathmini maeneo ya ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea. 

Amebainisha kuwa TFRA inajumuisha wakufunzi wa MATI katika programu zake za mafunzo kwa wakulima, ili kuwawezesha wakufunzi hao kuendeleza utoaji wa elimu kwa wakulima kwa ufanisi pindi mafunzo yanapohitajika.

Katika wasilisho lake, Meneja wa TARI – Maruku, Dkt. Mpoki Shimwela, ameeleza kuwa, matumizi duni ya mbolea katika kilimo cha migomba yamesababisha upungufu wa virutubisho kwenye udongo, hali inayochangia kuzalisha ndizi kilo chache na zisizo na ubora unaokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa

Alibainisha kuwa, TARI imeanzisha miradi mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya mbolea, ikiwa ni pamoja na vipimo vya afya ya udongo kwa wakulima ili kuwasaidia kuelewa mahitaji halisi ya udongo wao.

Shaban Mkulila, mkulima wa kahawa kutoka Kijiji cha Maruku, baada ya kutembelewa na Bodi na menejimenti ya TFRA shambani kwake Maruku ameeleza kuwa, tangu aanze kutumia mbolea katika kilimo cha kahawa mwaka 2019, ameshuhudia ongezeko kubwa la mavuno. 

Ameishauri TFRA kuanzisha mashamba darasa ili wakulima wapate mafunzo kwa vitendo na kuwasaidia kuondokana na dhana potofu kwamba mbolea inaharibu udongo.

Naye, Bw. Siraji Amri, mkulima wa kahawa kutoka Kijiji cha Mulata, Kata ya Katerero, amethibitisha kuwa matumizi ya mbolea za viwandani yamemwezesha kuongeza uzalishaji hadi kufikia wastani wa kilo sita za kahawa kwa kila mti mmoja, hali inayothibitisha mchango wa mbolea katika kuimarisha tija ya kilimo.

Ziara hiyo imetoa mwangaza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya TFRA na taasisi za kilimo katika kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu matumizi ya mbolea kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kufanikisha azma ya kilimo biashara nchini.

 Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na kampuni za mbolea za ETG na Itracom zimefanikiwa kusambaza tani nne za mbolea kwa ajili ya kutoa elimu kwa vitendo kupitia mashamba ya mfano yaliyoanzishwa katika Halmashauri zote za mikoa ya Lindi na Mtwara.


Elimu hiyo inalenga kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea kwenye shughuli zao za ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Hadi kufikia Januari 2025, mafunzo kwa vitendo yamefanyika katika Halmashauri za Mtwara Vijijini, Newala, Masasi DC, Masasi TC, Ruangwa, Mtama, Lindi MC, na Kilwa.

Mashamba hayo ya mfano yanawawezesha wakulima kujifunza matumizi sahihi ya mbolea na mbinu bora za kilimo, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa kilimo kinachozingatia kanuni bora za kilimo kunakopelekea kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula katika mikoa hiyo.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Afisa Kilimo Mwandamizi wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Ali Linjenje, alisema kuwa, mkoa wake umelenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 433,000 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia tani 616,000 msimu wa 2024/2025.

Aliongeza kuwa, hamasa kubwa inahitajika kwa wakulima, hasa katika matumizi ya mbolea, ili kufanikisha lengo hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Bw. Abeid Kafunda, aliahidi kushirikiana kwa karibu na TFRA katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kupitia mashamba ya mfano.

Bw. Kafunda alisema, ni aibu kwa Mkoa wa Mtwara kutegemea chakula kama mchele kutoka mikoa jirani kama Morogoro na Pwani, ilhali tuna ardhi nzuri inayofaa kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.

Naye, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Bw. Swalehe Mkuwili, alisisitiza kuwa, TFRA itaendelea kushirikiana na Halmashauri zote za mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea moja kwa moja kupitia mashamba ya mfano.

Hatua hii iliyochukuliwa na Mamlaka ni utekelezaji ya maelekezo ya Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, aliyoyatoa Oktoba 2, 2024, wakati wa ziara yake mikoa ya Lindi na Mtwara.

Waziri alihimiza TFRA kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kampuni za mbolea ili kuongeza kasi ya matumizi ya mbolea na kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya chakula unaongezeka katika mikoa hiyo.



 WAKALA wa Taifa wa hifadhi ya chakula(NFRA)Kanda ya Songea mkoani Ruvuma,imenunua tani zaidi ya 72,000 za mahindi kutoka kwa wakulima katika msimu wa kilimo 2024/2025.


Meneja wa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula kanda ya Songea Zenobius Kahere amesema,mahindi hayo yamenunuliwa kupitia vituo 21 vilivyowekwa katika Halmashauri saba za mkoa huo isipokuwa wilaya ya Tunduru ambayo sehemu kubwa wananchi wake wanajishughulisha na kilimo cha zao la korosho.

Kahere alisema, kwa kuwa mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa iliyopewa hadhi ya kuwa ghala la Taifa kutokana na uwezo wake katika uzalishaji wa zao hilo na mazao mengine ya chakula na biashara,wakati mwingine NFRA inahudumia mikoa mingine yenye upungufu wa chakula hapa nchini.

“Tulifungua vituo vya ununuzi katika Halmashauri zetu saba kati ya nane na tuliweza kukusanya mahindi zaidi ya tani hizo elfu sabini na mbili,ilipofika mwezi Novemba vituo hivyo vilifungwa na kazi inayoendelea kwa sasa ni ukusanyaji na ubebaji wa mahindi hayo kutoka kwenye vituo na kupeleka kwenye maghala mbalimbali kwa ajili ya kuhifadhi”alisema Kahere.

Alisema,katika msimu wa mwaka huu wakulima wa mahindi walifurahia bei nzuri ya Sh. 700 iliyotolewa na Serikali ikilinganisha na bei ya watu binafsi ambaao walinunua kati ya Sh.300 hadi 450 kwa kilo moja.

Hata hivyo alisema, changamoto kubwa iliyojitokeza ni ubora wa mahindi yaliyopelekwa sokoni na wakulima kutoka katika maeneo mbalimbali kwani hayakuwa na ubora hivyo kukosa vigezo vilivyowekwa na NFRA.

Alisema,hali hiyo iliwalazimu wakulima kutumia muda mrefu kukaa kwenye vituo vya ununuzi kwa ajili ya kusafisha na kuchagua ili kupata mahindi yenye ubora kabla ya kupokelewa na kupimwa.

Alisema kutokana na changamoto hiyo, katika msimu wa kilimo 2025/2026 NFRA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa wakulima kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia ikiwemo matumizi ya mbegu bora,kufuata kanuni kuanzia hatua za awali za kupanda hadi wakati wa mavuno.

Kwa mujibu wa Kahere,hatua hiyo itawasaidia wakulima kupata mahindi yenye ubora yanakayokidhi viwango ili kuepuka hasara,kuingia gharama kubwa kwa ajili ya kusafisha na kupoteza muda mwingi kwenye vituo vya ununuzi.

Amewataka wakulima,kuzingatia na kufuata maelekezo ya maafisa ugani na wataalam wengine wa kilimo wakati huu wanapoanza maandalizi ya msimu mpya wa kilimo ili waweze kupata mavuno mengi yatakayokubalika sokoni.

“Wakulima wasisite wala kuogopa kuwatumia maafisa ugani waliopo kwenye maeneo yao kwa ajili ya kupata ushauri wa kilimo cha kisasa badala ya kuendelea kulima kwa mazoea”alisisitiza Kahere.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya siku saba mkoani Ruvuma,aliwapongeza wakulima kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuzalisha mazao kwa wingi na kuifanya Tanzania kuwa na usalama na uhakika wa chakula.

Aliwataka wakulima kuepuka kuuza kwa bei za walanguzi ya Sh.300, badala yake kuhakikisha wanauza mahindi yao kwa bei elekezi iliyotangazwa na Serikali ambayo ni Sh.700 kwa kilo moja.

Baadhi ya wakulima wa mahindi katika kijiji cha Kigonsera wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,walipokuwa wakisubiri kupima mahindi yao kwa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) kanda ya Songea katika kituo cha Kigonsera hivi karibuni.

Meneja wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA)Kanda ya Songea mkoani Ruvuma  Zenobius Kahere,akizungumza na baadhi ya wakulima wa mahindi katika kijiji cha Kigonsera wilayani Mbinga wakati wa msimu wa ununuzi wa mahindi uliomalizika mwezi Novemba mwaka huu,kushoto kwake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Andrew Mbunda.
Wakulima wa mahindi kutoka vijiji mbalimbali wilaya ya Namtumbo wakisafisha mahindi yao kabla ya kuuza kwa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA)kituo cha Rwinga wilayani humo,kushoto ni msimamizi wa kituo hicho kutoka NFRA Thabitha Mpangala.



MKURUGENZI Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliji (NIRC), Raymond Mndolwa, amewataka Wakandarasi wanaojenga miundombinu ya umwagiliaji kuhakikisha wanasaidia jamii hususani maeneo yenye miradi.

Mndolwa amesema hayo katika ziara ya ukaguzi na ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi ya umwagiliaji katika kata ya Mwamkulu wilayani Mpanda mkoani Katavi.

Katika ziara hiyo  alikagua na kutoa maelekezo kwa wasimamizi wa miradi pamoja na Wakandarasi, kuwa lengo la serikali ni kusaidia jamii hivyo pamoja na ujenzi wa miradi wakandarasi waone haja ya kutoa misaada maeneo ya miradi.

Aidha ameelekeza mradi wa Mwamkulu, mkandarasi ambaye ni kampuni ya M/S SICHUAN ROAD AND BRIDGE (GROUP) CORPORATION LIMITED ya Dar es Salaam, ambayo ndiyo inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika kata ya Mwamkulu aweze kusaidia ukarabati wa miundombinu ya Msingi ikiwemo nyumba ya muuguzi wa zahanati ya Mwamkulu na kutoa msaada wa vifaa katika shule za msingi zilizopo katika eneo la mradi ndani ya kata ya Mwamkulu.

Pia alisema kwa upande wa Tume, itakarabati jengo la kituo cha kutolea huduma za afya kwa wanawake na watoto na nyumba ya Mkunga katika zahanati hiyo ya kata ya Mwamkulu.

Katika ziara hiyo Mndolwa ameridhishwa na mwenendo wa kazi za ujenzi na kusisitiza kasi ya kukamilika kwa miradi hiyo kwa muhimu wa makubaliano ili wananchi waweze kunufaika.

Naye, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Katavi, Samson Bai, amefafanua kwamba, Miradi ya Umwagiliaji inayoendelea kujengwa katika kata ya Mwamkulu ni pamoja na mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu wenye thamani ya Shilingi bilioni 31.6 ambao utanufaisha jumla ya wakulima 1300 pamoja na ukarabati wa skimu ya Umwagiliaji Kabage wenye  gharama ya bilioni 23.

Aidha ujenzi huo unajuimuisha ujenzi wa mifereji ya kusakafia ndani ya eneo la hekta 3500 kwa upande wa Mwamkulu na mitaro kama hiyo katika eneo lenye ukubwa wa hekta 2500 upande wa Kabage pamoja na ujenzi wa mabanio.

Pia, ujenzi wa mradi huo utahusisha ujenzi wa barabara yenye jumla ya urefu wa km 90 ndani ya eneo la mradi na ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao, lenye uwezo wa kuhifadhi tani 4000 za mazao.  

Ukaguzi huo wa miradi ya Umwagiliaji umehudhuriwa na Mjumbe wa Bodi Bi. Anna Mwangamilo pamoja na Wakurugenzi na baadhi ya wakuu wa idara na Vitengo kutoka Makao Makuu ya Tume ya Taifa  Umwagiliaji.



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi katika Shule ya Sekondari iliyojengwa kwa fedha za Serikali iliyopo katika Kijiji cha Ihanda, Kata ya Mlali inayotarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwaka huu. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema na kulia ni Bw. Omary Nkullo.

SERIKALI imehimiza matumizi ya mbolea kwa wananchi wa Kijiji cha Mlali Iyegu kilichopo Kata ya Mlali katika Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma ili kuepuka upungufu wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa wingi kwa kutumia mbolea inayotolewa kama ruzuku kutoka Serikalini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokua akiongea na wananchi hao wakati wa ziara yake iliyolenga kusisitiza utunzaji wa mazingira, kilimo na kukahamasisha agenda ya elimu.

“Asilimia 90 ya Wakazi wa Kongwa ni wakulima na wanategemea kilimo kuendesha maisha yao. Nawasisitiza kufanya kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea kwani Serikali imeamua kuwapunguzia mzigo wa gharama kwa kuchangia asilimia 70 ya gharama hizo. Hakuna Serikali inayotaka kudhuru watu wake, mbolea inayotolewa ni bora na imepimwa kitaalamu. Hatutarajii kupata maombi ya chakula cha msaada kutoka Serikalini wakati uwezekano wa kutumia pembejeo bora na kupata chakula cha kutosha upo” Amesema Mhe Senyamule.

Katika ziara hiyo pia, Mhe. Senyamule aliweza kutembelea shule mpya ya Sekondari iliyojengwa kwa fedha za Serikali iliyopo katika Kijiji cha Ihanda, Kata ya Mlali inayotarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwaka huu. Shule hii inatarajiwa kuwa msaada kwa wanafunzi wa Kijiji hicho ambao walikua wakitembea umbali mrefu wa takribani kilometa 12 kila siku kwenda na kurudi.

“Nimefurahishwa na ukamilishwaji wa shule hii ambayo itaepusha watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule ya Sekondari Mlali. Serikali imetimiza wajibu wake hapa na wazazi mtimize wajibu wenu wa kuhakikisha watoto wanafika hapa shuleni” Amesisitiza Mhe Senyamule

Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Remidius Mwema, amesema kuwa walipokea fedha za ujenzi wa madarasa 70 katika Wilaya yake na yote yamekamilika hivyo watahakikisha watoto wote 7,719 wanaotarajiwa kuanza shule mwaka 2023, wanawasili shuleni. “Tumeweka jitihada za uandikishwaji wa shule za awali na msingi kwa kwa kuhimiza mabalozi na wenyeviti wa Mitaa kutembea nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila mtoto anayestahili kwenda shule anakwenda”

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa Bw. White Zuberi amesisitiza suala la elimu kwa kusema; “Tumetumia fedha za Madarasa kujenga shule mbili ikiwemo hii ya Ihanda, Mhe. Rais anawasaidia watu wa chini kuweza kusoma mpaka ngazi ya juu kwa kutoa elimu bure kuanzia awali hadi kidato cha sita, hivyo tuunge mkono juhudi za Rais kwa kupeleka watoto shule”

Kwa upande wa sekta ya mazingira, Mhe. Senyamule ameendelea kuhimiza kampeni yake aliyoizindua Desemba 31 mwaka Jana kwa kuwataka wanakongwa kupanda miti ya kutosha na kutunza vyanzo vya maji pia kuepuka ukataji miti holela. Sambamba na hilo, alionyesha mfano kwa kupanda Miti kwenye eneo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na eneo la shule ya Sekondari Ihanda kama ishara ya kusisitiza wananchi kupanda miti na akasisitiza Wilaya hiyo kuhakikisha inafikia lengo la agizo la Serikali la kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kwa mwaka.

Vilevile katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alitembelea mradi wa ujenzi wa kituo mahiri cha nafaka kilichopo eneo la Mtanana ambacho kitakua na utaalamu wa kuzuia sumu kuvu kwenye mazao. Mradi huu upo chini ya Wizara ya Kilimo na unagharimu takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 19.

“Nimepata taarifa kituo hiki ni kikubwa Afrika Mashariki na kati, kitawezesha mazao yetu kuuzika kimataifa. Nimefarijika kusikia kuwa kituo hiki kitatoa mafunzo, hivyo naamini kitatoa darasa tosha. Naahidi sisi kama Mkoa, tutaendelea kusimamia mradi huu ili ukamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa” Amesema Mhe. Senyamule.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kongwa Bw. Omary Nkullo, amesema kujengwa kwa kituo hiki ni kutokana na historia iliyotokea miaka mitano iliyopita ambapo Mkoa ulipata vifo vya watu na wanyama kutokana na kula sumu kuvu kwenye mazao hivyo Wizara iliandaa mpango wa kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi na eneo hili tulihamisha wananchi kwa fidia ya Shilingi Milioni 8 hadi 9 na hati ya umiliki ikakabidhiwa Wizara ya Kilimo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki.



Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mlali, Wilayani Kongwa. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ambae alitoa fursa ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo na kuzipatia ufumbuzi, mkutano huo umefanyika mwishoni mwa wiki.

  

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo mahiri cha usimamizi wa mazao na nafaka kilichopo katika Kata ya Mtanana, Wilaya ya Kongwa. Kituo hicho kitakua na utaalamu wa kuzuia sumu kuvu kwenye mazao na ujenzi wake unagharimu takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 19. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema



 


Na John Walter-Manyara


Wakulima mkoani Manyara wameiomba Serikali kuangalia namna ya kusambaza  mbolea ya ruzuku  kutokana na usumbufu wanaoupata kwa kukosekana vituo vya karibu.


Wakizungumza na kituo cha redio cha Smile Fm, baadhi ya wakulima kutoka Dareda, Mamire  na maeneo mengine ya wilaya ya Babati wanasema wanatumia gharama kubwa kwa ajili ya usafiri kufuata Mbolea Mjini Babati huku wakieleza kwao hawaoni unafuu licha ya ruzuku iliyotangazwa na Serikali.


Changamoto nyingine waliyoitaja wakulima hao ni kupata namba ya malipo kwa wakati pamoja na mfumo wa kutambua orodha ya walioandikishwa kusuasua ilihali msimu wa kilimo umefika.

 

Ofisa Kilimo mkoa wa Manyara Paulina Joseph, alikiri changamoto hiyo kujitokeza kwa wakulima na kuahidi wataangalia namna ya kuongeza mawakala maeneo ya karibu na kueleza kuwa tayari wameweka mawakala wilaya ya Babati, Hanang’, Mbulu,Kiteto na Simanjiro.

 

Amesema pembejeo zingine kama mbegu zipo karibu kila eneo changamoto ni kwenye mbolea pekee hivyo wakulima waifuate mbolea hiyo inapopatikana ili wasipitwe na msimu wa kilimo wakati serikali inatafuta utatuzi.

 

Amesema serikali imeamua kuwaandikisha wakulima wote na kuwapatia ruzuku ya mbolea kwa bei nafuu ya shilingi 70,000 kutoka bei ya zamani 150,000 ili mkulima alime kwa tija na kuwa na uhakika wa chakula.