WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameitaka Afrika kujenga uwezo wake wa ndani wa kugharamia, kusimamia na kuzalisha mahitaji muhimu ya huduma za afya, badala ya kutegemea misaada na mifumo ya nje kwa muda mrefu.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo, Jumatano Septemba 09, 2026, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi unaofanyika jijini Arusha, ukiwakutanisha zaidi ya washiriki 2,700 kutoka mataifa 27.
Amesema Afrika inapaswa kubadili namna inavyoelewa na kutekeleza dhana ya kujenga uwezo, akisisitiza kuwa haipaswi kuishia katika miradi midogo isiyojenga uwezo wa kudumu, bali iwekeze katika uzalishaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia na wataalamu.
“Enzi zile nikiwa Waziri wa Fedha nilikuwa nawaambia nchi za Afrika zimeshashuhudia muda mrefu sasa wa maisha ya misaada na misaada inayoelekezwa pengine katika maeneo ambayo yanatofautiana na malengo ya ndani ya nchi kwa jina la capacity building. Capacity building. Capacity building. Na ndio tunaishia chapati, mandazi, sambusa. Hatuwekezi kitu kitakachodumu na kikawa endelevu.”
Dkt. Mwigulu amesema malengo ya ndani ya nchi yanayokwenda sambamba na malengo ya maendeleo endelevu yanapaswa kuheshimiwa na washirika wa maendeleo, ili misaada na uwekezaji viweze kuacha matokeo ya kudumu katika maisha ya Waafrika.
Amesema Tanzania inaendelea kuweka nguvu katika kuimarisha huduma za afya, ikiwemo kuongeza miundombinu, rasilimali watu na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ambayo Serikali imeanza kutekeleza mwaka 2026.
“Tunapozungumza kuhusu afya ya msingi, tusizungumzie tu kujenga vituo vya afya. Tujenge pia uwezo wa nchi zetu kugharamia huduma hizo, kuzalisha mahitaji yake na kutumia teknolojia zetu wenyewe,” amesema.
Aidha, amesema Tanzania imeanza kuwekeza katika uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa ili kupunguza utegemezi wa misaada na kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaendelea kuwa wa uhakika hata wakati dunia inapokumbwa na changamoto zinazoathiri minyororo ya usambazaji.
Amesema Serikali pia itaendelea kuboresha mazingira ya watumishi wa afya, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za watumishi na kuongeza ajira katika sekta hiyo.
Dkt. Mwigulu amesema mkutano huo unapaswa kuzaa hatua mahsusi zinazoweza kutekelezwa na kupimwa, badala ya kuishia katika mijadala na maazimio.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, amesema Afrika ya mwaka 2026 si Afrika ya mwaka 1960 na kwamba wakati umefika kwa washirika wa maendeleo kubadili namna wanavyoshirikiana na serikali za Afrika.
Dkt. Kaseya amesema serikali za Afrika zinapaswa kuwa na umiliki na uelewa wa rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya afya, huku fedha za washirika zikiendana na mipango ya kitaifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO, Profesa Mohammed Janabi, amesema changamoto kubwa si kukosa suluhisho, bali ni kukosa ujasiri wa kuyafadhili, nidhamu ya kuyatekeleza na uwajibikaji wa kuyadumisha.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amesema Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuwa ndiyo ngazi inayohudumia wananchi wengi zaidi.
Amesema asilimia 95.6 ya wajawazito wanaojifungua nchini wanapata huduma katika ngazi ya afya ya msingi, huku asilimia 86 ya mahudhurio ya wagonjwa wa nje katika vituo vya umma yakihudumiwa katika ngazi hiyo.
Profesa Shemdoe amesema kati ya vituo 8,288 vya afya vinavyomilikiwa na Serikali, vituo 7,946 sawa na asilimia 95.8 ni vya ngazi ya afya ya msingi, hivyo uwekezaji katika ngazi hiyo ni uwekezaji wa moja kwa moja kwa wananchi wengi.
Mkutano huo wa siku tatu unajadili namna ya kuimarisha huduma za afya ya msingi kuelekea upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kupitia ufadhili endelevu, ufanisi, ubora wa huduma, ubunifu, ushirikiano wa kikanda na kujenga mifumo ya afya inayostahimili majanga.















Post A Comment: