CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha kimewataka wanachama wa cha hicho kupuuza taarifa za upotoshaji zilizotolewa na moja ya mitandao ya kijamii hapa nchini kuwa kimemnyima ofisi mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Maganya  Fadhili kwa ajili ya kufanya mkutano wake na waandishi wa habari mkoani hapa.

Aidha kimeseama kitaendelea kumpa ushirikiano mwenyekiti huyo wakati wowote atapokuwa Arusha kwa maslahi mapana ya Jumuiya hiyo na CCM kwa jumla.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Arusha Gerald Munisi amesema taarifa hizo hazina ukweli ndani yake na kuwataka wananchi na wana CCM kuzipuuza kwa sababu majungu na fitina zenye nia ovu ya kutaka kuwagawa wana CCM na viongozi wake.

Amesema Fadhili alifanya mkutano wake na waandishi wa habari  kwenye ukumbi wa CCM mkoa wa Arusha wa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu waandishi walikuwa 37 hivyo ingekuwa vigumu kuenea kwenye ofisi moja.

Munisi amewataka waandishi wa habari mkoani hapa iwapo wana jambo lolote ambalo wanahitaji ufafanuzi ni vyema wakawasiliana naye au Katibu wa CCM mkoa wa Arusha badala ya kuandika habari ambazo hazina weledi.

Awali Fadhili Maganya ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alisema ataendelea kushirikiana na uongozi wa CCM mkoa wa Arusha kwa kuwa wao ni wamoja na kwamba siasa za Arusha zinajulikana na kwamba hazitapata nafasi kamwe ya kuwagombanisha viongozi katika Mkoa huo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Zelothe Steven alisema wataendelea kumpa Fadhili ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha majukumu yake ya kikazi akiwa ndani na nje ya Mkoa wa Arusha ikiwa ni pamoja na kuisimamia Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Arusha kutekeleza majukumu yake kikamilifu.


Share To:

Post A Comment: