Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Masoud Othman akipata maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru Dauson Malela ya namna bunifu bora na ya kipekee ya zana rahisi ya kupandia pamba maarufu 'Rafiki Planter' inavyofanya kazi. Tukio hilo lilitokea kwenye Maonesho ya Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika jijini Dodoma.

Na Godwin Myovela 

WATAFITI kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru wapo kwenye mchakato wa maboresho ya bunifu yao ya zana rahisi na ya kipekee ya kupandia pamba maarufu 'Rafiki Planter' kutoka hatua ya kukokotwa na wanyama na kuvutwa na binadamu na sasa kuwekewa viongeza mwendo (motorised machines) ili kuongeza ufanisi.

Zana hiyo ambayo imegeuka mkombozi kwa wakulima wa pamba kwa kurahisisha shughuli zote za upandaji, ina uwezo wa kutumia kati ya saa moja mpaka masaa 3 kupanda eneo la ekari moja, ikilinganishwa na wastani wa masaa kati ya 10 na 11 ambayo hutumika kama zao hilo litapandwa kwa mkono.

Aidha, zana hiyo inapokuwa inakokotwa au kuvutwa na binadamu kupitia sehemu maalum ya kufunga mnyororo  au mkono wake wa kuvuta, ina uwezo wa kudondosha mbegu kutoka shimo hadi shimo kwa cm 30, na kutoka mstari hadi mstari cm 60, sanjari na uwezo wa kubeba mbegu kati ya kilo 3 mpaka  6 kupitia vibeba mbegu maalum kwa wakati mmoja.

Pia ugunduzi huo, umeiwezesha zana hiyo kuwa na uwezo mahsusi ya kutengeneza yenyewe mashimo ya mbegu na vifukia udongo ambavyo hufanya kazi yake punde tu mbegu inapodondoshwa.

Kwa mujibu wa Tari, teknolojia ya zana hiyo imewekewa mfumo wa vifungua ardhi ambavyo kadiri zana hiyo itakavyokuwa inasogea vifungua ardhi hivyo vinachimba mashimo  kwa maana ya kutengeneza mifereji kwa umbali wa cm 60 kutoka kimoja hadi kingine.

Mkurugenzi wa kituo hicho, ambaye pia ni mratibu wa zao la pamba nchini, Dk. Paul Saidia alisema ugunduzi huo na maboresho yake vitahusisha, kushawishi na kuvutia idadi kubwa ya makundi mbalimbali wakiwemo vijana, wanawake na wazee kuingia katika kilimo tofauti na ilivyokuwa awali, na hivyo kuongeza tija zaidi ya mara mbili kwenye uzalishaji wa pamba.

Akizungumza jijini hapa, wakati akishiriki utekelezaji wa mradi wa kuinua thamani kwenye mnyororo wa zao la pamba unaojulikana kama 'Beyond Cotton,' Saidia alisema kabla ya uwepo wa zana hiyo, na baada ya kufanya majaribio walibaini nguvu kazi ya wakulima kati ya 12 na 14 ilitumika kupanda ekari moja kwa siku 1 kwa wastani wa masaa 10 hadi 11.

Aidha, alisema hali hiyo hata hivyo ilipelekea usumbufu kwa wakulima walio wengi kutumia muda mrefu kutengeneza kamba, kunyoosha mstari na kuweka vipimo kwa kutumia zana duni za jembe la mkono sambamba na kuinama kwa muda mrefu, hususan wakati wa kudondosha mbegu na kufukia, hali iliyosababisha ugumu kwenye kufikia azma ya uzalishaji wa pamba kwa tija.

"Sasa naamini bunifu hii ni mkombozi  sababu inafanya kazi zote tatu; kwa maana ya kuchimba mashimo yenyewe, kuweka mbegu na kufukia. Pia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Tume ya Sayansi Teknolojia Bodi ya Pamba nchini  tupo kwenye mchakato wa kuifanyia maboresho kwa kuifungia 'motorised machine' itakayotumia mafuta ya petrol ili kuipa ufanisi zaidi," alisema Dk. Saidia.

Zaidi alisisitiza; "Kilichopelekea wazo la uvumbuzi huu ilikuwa ni baada ya tafiti nyingi za kubadilisha namna ya upandaji pamba kutoka kwenye cm 90 kwa 40 wa hapo awali kuja kwenye huu mpya wa sasa wa  cm 60 kwa 30 kufanywa kupitia mradi wa 'Cotton Victoria' katika azimio lililofanyika kwenye mkutano wa wadau mkoani Simiyu mwaka 2020."

Ikimbukwe, katika mkutano huo ilionekana upandaji mpya wa cm 60/30 pamoja na uzuri wake lakini bado ulikuwa na changamoto ya matumizi makubwa ya muda, ongezeko la nguvukazi na idadi ya mimea. Mathalani upandaji wa cm 90/40 ililazimika kuwa na mashimo yapatayo 11,111 kwa ekari, wakati 60/30 idadi ya mashimo ya kupandia mbegu ni 22,222.

Kwa mantiki hiyo, kwenye kila shimo au mashimo zinapopandwa zaidi ya mbegu 2 kitaalamu inashauriwa mkulima ang'olee ili ibakie mimea 2; na kwa kufanya hivyo, idadi ya upandaji wa awali wa cm 90/40 kwa mashimo 11,111 mimea itakuwa 22,222, na upandaji wa sasa ulioidhinishwa nao mimea itaongezeka mara mbili zaidi kutoka 22,222 hadi idadi mpya ya 44, 444 kama itang'olewa na kubakizwa miwili kwa kila shimo.

Kwa upande wake mmoja wa wataalamu kutoka Idara ya Uhaulishaji Teknolojia ambaye pia ni miongoni watafiti wavumbuzi wa zana hiyo kutokaTari Ukiriguru, Dauson Malela alipongeza Taasisi za Bodi ya Pamba nchini (TCB), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) , Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) pamoja na  kiwanda cha kuchambulia pamba cha Biosustain mkoani Singida kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika kufanikisha uvumbuzi wa zana hiyo.

Kwasasa Costech kwa kushirikiana na Tari wapo kwenye mchakato wa majaribio kadhaa ya kuboresha zana hiyo kutoka kwenye mfumo wa sasa kwenda kwenye hatua kubwa zaidi ya kufungia mashine itakayowezesha kujikokota yenyewe, ili hatimaye iwe  rahisi zaidi na rafiki kwa wakulima wasio na mifugo na wazee wasioweza kuivuta.

Uvumbuzi wa zana hiyo unakwenda sambamba na falsafa ya sasa ya Wizara ya Kilimo na Taasisi ya Utafiti nchini chini ya Waziri mwenye dhamana Hussein Bashe ambaye mara kadhaa amekuwa akitoa maelekezo mahususi kwa wataalam wa kilimo kuhakikisha wanaongeza kasi ya kiutendaji na tafiti ili kuleta mageuzi chanya ndani ya sekta hiyo katika kufanikisha ajenda ya 10/30.

"Mchakato wa maboresho kwenye zana hii mali ya TARI ambayo imegunduliwa na watafiti watatu Dk. Paul Saidia, Dauson Malela na Robert Chaleo unaendelea, pia tunakaribisha wadau wengine kujitokeza ili kwa pamoja tuweze kuinua tija ya kilimo cha pamba," alisema Malela.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru na Mratibu wa zao la pamba Tanzania Dk. Paul Saidia akielezea sababu zilizopelekea watafiti wa kituo hicho kubuni teknolojia hiyo rahisi na rafiki ya kupandia pamba maarufu 'rafiki planter.' 

Mtaalamu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Ukiriguru Dauson Malela akionyesha zana hiyo waandishi wa habari waliofika kituoni hapo (hawapo pichani) 

Mwonekano wa zana hiyo.

Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.

Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.

Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.

Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.

Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani.

Mwonekano wa zana hiyo na namna inavyotumika ikiwa shambani

Kabla ya ugunduzi wa zana hiyo hali halisi ni kama inavyoonekana pichani kwa wakulima wa pamba kutumia muda mrefu kutengeneza kamba, kunyoosha mstari, kuweka alama na vipimo, kuchimba mashimo, kudondosha mbegu na kuzifukia kwa kutumia jembe la mkono jambo lililopelekea vijana wengi, wanawake na wazee kukata tamaa na kutafuta shughuli nyingine. Hivyo bunifu hiyo sasa ni mwarobaini wa changamoto hizo.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: