Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaolazimika kuhama makazi yao kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ni wanawake.

Kutokana na majukumu yao kama walezi na wanaohudumia familia kwa karibu zaidi huwafanya kuwa katika mazingira hatari zaidi wakati wa mafuriko na ukame unapotokea.

Hali hii ipo tofauti katika Kijiji cha Ndepesi Kata ya Orubomba Wilayani Longido ambako wanaume ndio wanaongoza kwa kuhama na kuacha familia zao. Wanaume hawa, huondoka nyumani ili kutafuta malisho ya mifugo katika Wilaya za jirani kama Simanjiro huku wakiwaacha wake zao wakiendelea kulea familia zao. 

Nabolo Lekibora ni Mama wa watoto sita (6), mkazi wa Kijiji cha Ndepesi anasema wao  kama wanawake wanaumia na kuteswa sana na mabadiliko ya tabia nchi hasa msimu wa kiangazi kwani wanatumia muda mwingi kutafuta maji. Ikiwa ni saa kumi na mbili asubuhi, Nabolo anasema

"Nimewahi kuja kutafuta maji hapa, nimeacha watoto wamelala na wakiamka watajiandaa kwenda shule bila hata kunywa chai maana wanaume wetu wamehamia West Kilimanjaro na Wilayani Simanjiro kwa ajili ya kwenda kutafutia ngombe malisho tumebaki sisi wakina mama wenyewe na familia zetu."

Amesema anaamka saa kumi na mbili kwenda kuwahi foleni ya maji  maana kila mwanamama anakuja na Punda wa kubebea maji na anaongozana na mbuzi na kondoo kwa ajili ya kuja kuwanywesha maji.

"Ninakaa hapa mpaka saa nne nikitoka hapa nikifika nyumbani napika chai kwanza alafu nalala kwanza nipumzike mpaka saa saba ndio naamka na kwenda mashambani kwa ajili ya kutafuta kuni ili niweze kwenda kuziuza nipate kipato".

Nabolo hayuko peke yake, Mbaima Miromo ni mkazi wa Kijiji hicho ambaye ni mwanamke wa miaka 24. Mbaina, yeye ni mama wa watoto wanne (4) anaeleza namna ukame ulivyo waathiri na kulazimika kutafuta maji umbali mrefu wa zaidi ya kilomita tatu kutoka katika boma lake hadi kufika kituo cha kuchota maji.

"Sasahivi ukame umekua mkubwa nalazimika kutoka na nguo zangu kuja kufua hapa wakati nachota maji, na mifugo pia inapopata maji, chakula kimekuwa cha shida  sema Mungu anasaidia mchana tunakunywa uji ila usiku tunakula "Kiteke" (Uji mzito unaoelekea kuwa ugali lakini sio ugali kabisa)  ambao naweka tu chumvi na mafuta".

"Chai huwa napika usiku naweka kwenye chupa ili asubuhi watoto wakiamka weweze kunywa chai wakati mimi nakuja kupambana kutafuta maji lakini ikitokea kama hatuna maji kabisa basi watoto wanaenda shule hivyo hivyo bila kunywa chai".

Mbaina anaeleza “Mwanzoni nilikuwa naishi Kenya nimekuja nikakuta hii hali katika Kijiji chetu nimejaribu kuzungumza na Diwani na Mwenyekiti nimewaomba waangalie namna bora ambayo serikali itasaidia kufikiwa na huduma hii ya maji kwa kweli tunateseka na ukiangalia mifugo nayo haina chakula wakati pumba imekuwa ghali na hatuna fedha za kununua pumba tulishe mifugo yetu.”

Ally Msangi ni Mchumi wa Halmashauri ya Longido ambaye amejikita zaidi katika kusimamia masuala ya mabadiliko ya Tabia Nchi Wilayani humo. Ally anaeleza jinsi wanawake walivyothirika zaidi kutokana na eneo kubwa la Wilaya hiyo kuwa kame.

Anasema eneo likishakuwa kame upatikanaji wa maji unakuwa ni mgumu kwani wilaya nzima hakuna chanzo cha maji na wananchi wanategmea maji ya kwenye mabwawa, visima vya kuchimba na maji ya mradi kutoka Mto Simba uliopo West Kilimanjaro.

"Wanawake ndio watafutaji wa maji wakuu katika familia ukame umekuja umewaathiri sana mabwawa yamekauka wakina mama ambao walikuwa wanapata maji kwenye mabwawa ya karibu kwa sasa inawalazimu kutembea umbali mrefu kwa zaidi ya saa nne mpaka tano ili kupata huduma ya maji na kama atatumia muda wote huu kwenda kutafuta maji ni kwamba akirudi kuchota maji hataweza tena kwenda kwenye shughuli zake za kila siku za kujitafutia kipato na uzalishaji".

"Wakina mama wa Longido kwa sasa baada ya mbadiliko haya ya Tabia Nchi hawafanyi shughuli nyingine yoyote zaidi ya kutafuta maji,biashara za kwenye masoko na minada zimeanza kuzorota sana kwani wateja ni hawa hawa wafugaji wenyewe wananunua wana wauzia wenzao". Aliongeza Ally.

Mchumi huyo anaeleza kuwa  "Kama hali itaendelea kuwa hivi huko tuendako wananchi wengi watakufa kwa njaa na watoto wengi watapata utapiamlo na ugonjwa wa kupooza na watoto wa shule kuacha shule na kujiunga na wazazi wao kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya familia zao, idadi ya wananchi imeongezeka na wanyama pori nao wanatoka huko porini wanakuja kwenye makazi ya watu kutafuta maji ya kunywa".

Kwa upande wake, Nabolo Lekibora anaiomba serikali ya Rais Samia katika kauli yake ya kumtua mama ndoo kichwani kuwafikia wamama wa Ndepesi ili waweze kufikiwa na huduma ya maji safi na salama kwa ukaribu kwani wanatoka umbali mrefu zaidi ya kilomita tatu hadi nne kwenda kwenye kituo hicho cha maji na muda mwingine wakija wanakosa maji kabisa, pia serikali igawe chakula kwa jamii hiyo kwani ardhi yetu haifai kabisa kwa kilimo.

Mbaina anamaliza kwa kusema “Sisi kama jamii ya kifugaji tunaiomba serikali inapofanya zoezi la ugawaji wa miti itoe miti ya matunda ambayo inastahilimi ukame ambayo inayoleta uoto wa asili, pia kwa ndugu zetu wa mashirika kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kutumia nishati mbadala ikiwemo utengaji wa nyanda za malisho na kilimo bila kuwasahau nyie waandishi wa habari muendelee kuja kuripoti habari hizi zinazoibua changamoto kwa jamii ili tuweze kupatiwa ufumbuzi.”

Kwa upande wa serikali, wao wameanza kutoa elimu ya ufugaji bora na wa kisasa badala ya kufuga mifugo ambayo inahitaji maji mengi na eneo kubwa la malisho.

Watendaji wa serikali wanashauri badala ya kufuga ng’ombe wanaohitaji uwekezaji mkubwa, wafugaji wajikite katika ufugaji wa mbuzi, kondoo na kuku kwani mifugo hii inahitaji malisho kidogo na pia wanastahimili ukame.


Share To:

Post A Comment: