DENIS CHAMBI, TANGA.


Katika kuendelea kuwaelimisha na kuwarahisishia wananchi juu ya huduma ya Nikonekt ya shirika la umeme Tanzania  'TANESCO' mkoa wa Tanga imtoa mafunzo  maalum ya  ubalozi kwa waandishi wa habari wakiwa ni wadau muhimu katika shirika hilo ili kuendelea kuhabarisha jamii  kupata huduma zilizo Bora sambamba na kuwasaidia kuondokana na ulaghai wa watu ambao wamekuwa wakiwatoza fedha kwa maslahi yao binafsi.


Akizungumza mara baada ya kutoa mafunzo hayo afisa uhusiano na wateja   kutoka shirika la umeme Tanzania 'TANESCO' mkoa wa Tanga Amoni  Bidebuye alisema kuwa kwa kutambua mchango wa vyombo vya habari hapa nchini katika sekta hiyo kupitia huduma zinazotolewa na Tanesco wameona ipo haja kuwatumia waandishi wa habari ili kuwafikia wananchi popote walipo kuendelea kurahisisha  uboreshaji, upatikanaji na utoaji  wa huduma ambamba na kupambana na uharibifu wa miundombinu. 


"Tunataka waandishi wa habari wawe mabalozi katika mfumo wa uboreshwaji wa  uunganishaji wa umeme 'Nikonekt'  tunataka taarifa imfikie mteja popote pale alipo ili angalau kila mwananchi afahamu na aelewe Tanesco ipoje sasa, tumekubaliana kila mmoja atakuwa balozi , kutoa elimu ya namna  wateja watapata huduma kupitia mfumo wa kidijitali wa Nikonekt ambao hauna haja ya kufika Tanesco ili upate huduma"


"Na  hii huduma ya Nikonekt imekuja kutatua changamoto kubwa  iliyokuwa ikiwasumbua wateja wetu ambayo ilikuwa ili upate  huduma lazima uwe na mtu pale Tanesco au lazima utumie  mtu yeyote wa kati sasa Nikonek tukasema hapana unaweza ukapata huduma ukiwa hata nyumbani tunataka wananchi wajue kuwa sasa hivi kuunganishiwa umeme sio suala la kuwa unamfahamu nani" aliongeza Bidebuye.


Aidha afisa huyo alisema katika kuendelea kupambana na kutatua changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya umeme wameona ni vyema kuwatumia wanahabari katika kupata taarifa na kutoa elimu kwa wananchi juu ya ulinzi wa miundombinu  ili kuwa salama nyakati zote na kuendelea kutoa huduma.


"Lakini kubwa zaidi pia tumekubaliana kuwa mabalozi wa  usalama wa miundombinu kwa sababu imeonekana moja ya tatizo linaloleta changamoto kwenye suala kukatika kwa umeme ni kutokana na uharibifu wa miundombinu mtu akivamia na kuingilia umeme tayari umeme unakatika"


Afisa uhusiano huyo alibainisha kuwa huduma hiyo ya Nikonekt imekuja kuleta  mafanikio makubwa na kuondoa malalamiko tofauti na hapo awali kwani mara tu mteja anapokamilisha taratibu zote za kuomba huduma ya kuunganishiwa umeme taarifa zimekuwa zikiwafikia Tanesco na ndani ya siku tatu mwamachi hupatiwa huduma yake.


Akizungumzia suala la kutakika katika kwa umeme mara kwa mara  alisema mabadiliko ya tabia nchi yamechangia kwa kaisi kikubwa ikiwa ni pamoja na kukauka kwa mto uliopo Hale unaopeleka maji katika Bwawa la  Pangani ambapo amesema kuwa katika kupambana na changamoto hiyo zipo jitihada zilizoendelea kufanyika ikiwa pamoja na   kukarabati miundombinu iliyopo.


" Kuna miradi mbalimbali inaendelea kufanyika hapa nchini lakini sisi kama Tanga  tunahakikisha kuwa muda huu tunatumia kufanya matengenezo na tunatarajia muda sio mrefu tuwe tumemaliza  matengenezo ya njia zetu isije ikatokea tena mtu anakatiwa umeme ,na tunaendelea kufanya ukarabati na kuimarisha ulinzi maana mengine yanasababishwa na shughuli za kibinadamu mfano wanaolima karibu na miundombinu" alisema Bidebuye.


"Lakini pia mabadiliko ambayo tunatarajia  kuyafanyia ni kuchukua umeme kutokea Arusha   kuja Tanga kama hii  hali ya kukatika katika kwa umeme itaendelea  na hivyo kufikia mwezi wa kumi na mbili hadi wa kwanza  na hiyo itasaidia kuongeza  kiwango  cha umeme wa kutosheleza kwa mkoa wa Tanga" alisema Bidebuye.


Wakizungumza baadhi ya waandishi wa habari mara baada ya kupata elimu hiyo ya kuwa mabalozi wa Tanesco walisema kuwa kwa kutumia taaluma na kalamu zao wapo tayari kuelimisha wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo pamoja na kushirikiana  katika kulinda na kutunza miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali.


"Kwa kupitia kwetu sisi waandishi wa habari maswala mengi sana yataeleweka  kwasababu moja wapo ya matatizo ambayo yamekuwa yakitokea ni ukosefu wa elimu na taarifa  na hazifiki sehemu zinakotakiwa lakini sasa kwa kupitia vyombo vya habari itatusaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha  taarifa nasisi kwa kutumia utaalamu wetu katika kuwaelimisha watu" alisema George Semboni Mwandishi wa gazeti la Citizen.


" Sisi  kama mabalozi wa Tanesco hapa nchini na  hasa mkoa wa Tanga tunapongeza  jitihada zinazofanyika kuboresha upatikanaji wa umeme  na tunajua kabisa kwamba umeme ni tegemeo kubwa na  mkoa wa Tanga unakuwa ni tegemeo kubwa na fursa zote zipo tunaona kuna Barabara kubwa inatengenezwa ya kutoka Bagamoyo hadi Tanga  ujio wa Bomba la mafuta, upanuzi wa bandari ya Tanga kwa hivyo umeme ni nyenzo muhimu sana ya kukuza uchumi wa mkoa na Taifa" alisema Willium Mngazija mwandishi wa ITV.


MWISHO.

Share To:

Post A Comment: