MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 3, 2022 Jijini Dodoma,wakati akito taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Mamlaka hiyo kuanzia Julai 2021 hadi Septemba 2022.


  Na Janeth Raphael

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Kuwe amesema kuwa Uwiano baina ya mitandao na matumizi yanaonesha kuwa maeneo mengi yamefikiwa na huduma za Intanet ila watumiaji ni wachache hivyo kuna haja ya kuongeza upatikanaji wa simu janja.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Mamlaka hiyo kuanzia Julai 2021 hadi Septemba 2022 , mbele ya waandishi wa habari Novemba 3,2022,Jijini Dodoma ,Dkt.Jabir amesema kuwa Muelekeo wa kufikia lengo la serikali la asilimia 80 ya watumiaji wa huduma za Intanet ifikapo mwaka 2025 zinaendela vema.

"Tuna haja ya kuangalia nini kifanyike ikiwezekana kuongeza kwa kasi elimu ya matumizi ya simu janja na kuongeza upatikanaji wake kwa wananchi kwani Uwiano baina ya mitandao na matumizi yanaonesha kuwa maeneo mengi yamefikiwa na huduma za Intanet ila watumiaji ni wachache ,"Ameeleza Dkt.Jabir

Dkt.Jabir amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano ya Simu nchini imeendelea kukua na hadi kufikia Septemba, 2022 kulikuwa na laini za simu 58.1 Milioni, Idadi hii ya laini za simu inahusisha laini zinatotumiwa na watu na laini zinatumiwa kwa ajili ya mawasiliano kati ya mashine kwa mashine (M2M).

"Takwimu zinaonyesha kwamba mikoa mitano (5) Tanzania inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini za simu zinazotumika yaani (Active SIM-cards) hadi Septemba 2022 ni Dar es salaam (Laini Milioni 9,756,697), Mwanza (Laini 3,700,914), Arusha (3,448,200), Mbeya (3,089,848), na Tabora (3,060,407),"Amesema Dkt.Jabir

Dkt.Jabir amebainisha kuwa Takwimu za sasa zinaonesha kuwa matumizi ya Intaneti yameongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka milioni 29,858,759, mwaka 2021 hadi kufikia 31,122,163 mwezi Septemba 2022.

"Idadi ya watumiaji wa intaneti kwa sasa wamefikia 31,122,163,Mwelekeo wa ongezeko la watumiaji wa intaneti linaonesha kwamba kulikuwa na ukuaji wa takriban asilimia 17 kila mwaka, katika kipindi cha miaka 5 ambapo mwaka 2017, kulikuwa na watumiaji Milioni 16,106,636 na mwishoni mwa mwaka 2021 waliongezeka kufikia Milioni 29,103,482,

Na kuongeza kuwa "Ongezeko la matumizi ya intaneti limechangiwa pia na matumizi ya Kiswahili, Maudhui ya Kiswahili kwenye intaneti yanaongezeka kwa kasi na Program tumizi (applications) kwa lugha ya Kiswahili zimeongezeka pia,"Ameeleza Dkt.Jabir

Akizungumzia takwimu za ripoti ya utendaji wa sekta ya Mawasiliano nchini Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa kuna mitandao mitano (5) ya kijamii inayotumiwa zaidi, hivyo kuongoza kwa kiwango kikubwa cha data iliyotumika kwa kipimo cha GB; ambapo Mtandao wa kijamii wa FaceBook uliongoza kwa kurekodi (GB Bilioni 2.59), ukifuatiwa na YouTube wenye (GB Bilioni 1.91), kisha WhatsApp uliokuwa na (Bilioni 1.58), na TikTok ukiwa na (GB Milioni 999) ikifuatiwa na mitandao mingine.

Pia ,Dkt.Jabir amesema kuwa TCRA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kama UCSAF, Watoa huduma za mawasiliano, TANESCO, Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) pamoja na kuchangia katika Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ili kuhakikisha kuwa huduma za Mawasiliano zinafikishwa kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaendelea kusimamia Sekta ya Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali katika ngazi ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha Sekta ya Mawasiliano inatoa mchango katika maendeleo ya nchi na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa kidijiti na uchumi wa buluu.

Share To:

Post A Comment: