DENIS CHAMBI, TANGA. 

MASHINDANO ya michezo mbalimbali inayoyashirikisha mashirika , makampuni na Taasisi binafsi hapa nchini maarufu kama 'SHIMUTA' kwa mara ya kwanza tangu yaanzishwe , mwaka huu 2022 yameweka rekodi mpya kwa kuwa na timu zaidi ya 52 zikipepetana kutafuta mabingwa kupitia michezo watakayoshindanishwa. 

Michezo hiyo ambayo inahusisha timu za watumishi kutoka mashirika na taasisi binafsi inaanza kutimua vumbi leo November 15 katika viwanja tofauti tofauti huku ikitarajiwa kuzinduriwa rasmi na mlezi wa SHIMUTA ambaye ni makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt.Phillip Mpango November 21 hapa hapa mkoani Tanga. 

Mwenyekiti wa SHIMUTA taifa Roselyne Massam amesema tangu wameshika hatamu ya kuliongoza shirikisho hilo haijawahi kutokea kushirikisha timu nyingi zaidi kama mwaka huu jambo ambalo linaonyesha mwitikio umekuwa ni mkubwa na michezo hiyo kuonekana kuleta tija kwa washiriki mashirika, makampuni na taasisi zenyewe wanazotoka. 

"Ni kwa historia tangu tumeingia kwenye uongozi wa SHIMUTA, huu ni mwaka ambao tumekuwa na timu nyingi mwaka huu" alisema Roselyne. 

Mratibu mkuu wa shirikisho hilo Maswet Masinde amesema kuwa wamejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna mamluki yeyote atakayehusishwa kwenye timu zilitakazoshiriki jambo ambalo litaondoa kero na malalamiko ya hapa na pale kwa timu shiriki huku wakijipanga kusimamia sheria kanuni na taratibu zinazowaongoza katika michezo yote.

 "Tumefanya uhakiki kuondoa mamaluki katika mashindano yetu tumetumia taasisi za umma ikiwemo NHIF, WCF, PSSF kuhakiki washiriki lengo likiwa ni michezo hii iwe ni kwaajili ya watumishi wale ambao wanatambulika kisheria na ili uwe mshiriki unapewa leseni maalumu na lazima uwe umehakikiwa kwenye mifuko hiyo" alisema Masinde.

 "Tuna wanamichezo mpaka sasa hivi 2183 ambao tayari wameshafika hapa jiji la Tanga , kwahiyo ni namba kubwa sana ya wanamichezo wanaoshiriki, tuna kanuni ambayo inaongoza mashindano yetu lakini pia tutatumia kanuni za michezo husika pale inapobidi, tumeongea na waamuzi wasimamie sheria taratibu na miongozo inayoongoza michezo husika ili kusiwepo na manung'uniko ya hapa na pale" alisema

 Akiwakaribisha rasmi washiriki wa SHIMUTA mkuu wa mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema kuwa hali ya ulinzi na usalama iko shwari huku akiwataka wakazi wa Tanga ususan wafanyabiashata na wajasiriamali wafogo wadogo kutumia mashindano hayo kama fursa ya kujiongezea kipato. 

"Mashindano haya ni zaidi ya michezo yana faida ya kipato lakini yanainua uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuongeza pato la taifa, nitoe wito kwa wafanyabiashara wote wachangamikie fursa na kujitokeza kwa wingi katika michezo hii " alisema Mgumba.


 "Suala la hali ya ulinzi na usalama liko vizuri tumeendelea kuimarisha doria kwa sababu tumepata ujio wa watu wengi hivyo hali ya usalama iko vizuri tumeendelea kujiimarisha zaidi doria za mchana na usiku kuwahakikishia wanamichezo na wageni wetu wote wanakuwa salama wakati na hata baada ya kumaliza michezo" aliongeza

 Mashindano hayo yatashirikisha michezo ya mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa Pete , Wavu, Kikapu, Dats, Pool table, Vishale , Draft kukimbia kwa magunia, Riadha kuvuta kamba Bao na mingineyo kedekede, lengo kuu hasa ikiwa ni kuimarisha mahusiano baina ya taasisi, mashirika na makampuni kuimarisha afya kupitia michezo ikiwa pia ni kuondokana na magonjwa yasiyoambukiza. 

Michezo hiyo ambayo hufanyika kila mwaka ni kwa mara ya pili mfululizo kufanyika ndani ya mkoa wa Tanga mwaka huu yakija na kauli mbiu ya 'SHIMUTA familiya moja'.
Share To:

Post A Comment: