ZAIDI ya Sh bilioni 3.2 zimetumika katika Ujenzi wa jengo la utawala la ghorofa mbili la Halmashauri ya  Bumbuli, wilayani Lushoto, Tanga.

Jengo hilo ambalo litakuwa na vyumba 72 vya watumishi na wakuu wa idara zote za Halmashauri ya Bumbuli, linatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, wakati akitembelea miradi ya maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro alisema kuwa bajeti ya ujenzi wa ofisi za Halmashauri ni kiasi cha Sh bilioni 4 na ujenzi umefika asilimia 90.

Alisema kuwa Jimbo la Bumbuli lenye kilimo kikuu cha biashara ya chai lilikuwa halina ofisi za uhakika za halmashauri na ujenzi wa jengo la utawala ni juhudi za Mbunge wa Jimbo hilo Januari Makamba, ambaye pia ni Waziri wa Nishati.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Bumbuli na ikiwezekana pia siku ya kuzinduliwa kwa jengo hilo, mgeni rasmi awe Rais.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bumbuli, Magdalena Utouh, alisema kuwa jengo hilo limefika hatua za mwisho kwani linatakiwa kukabidhiwa Novemba 31 mwaka huu na fedha kwa ajili ya umaziaji ziko katika akaunti ya halmashauri.

Alisema jengo hilo ambalo ujenzi unatekelezwa na SUMA JKT, litakuwa jengo kubwa na la kisasa na wananchi wa jimbo hilo watakuwa wamezogezewa huduma karibu kwa maendeleo ya jimbo lao.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Lushoto, Ally Daffa aliishukuru serikali kwa kuhakikisha jimbo la Bumbuli linakuwa na jengo lenye hadhi la Halmashauri na kuwataka watumishi wa halmashuri hiyo kuhakikisha wanalitunza jengo hilo kwa maslahi yao wenyewe.

Share To:

Post A Comment: