Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso (Mb) ametembelea eneo la matengenezo ya bomba kubwa la inch 72 katika kata ya Wazo, Jijini Dar es salaam ambalo ni sehemu ya kimkakati ya kuongeza msukumo wa Maji katika Jijini Dar es salaam ili kukabiliana na hali ya kina cha maji kupungua na kuhakikisha matengenezo hayo yanakamilika.

Akiwa eneo hilo, Aweso ametumia nafasi hiyo kutoa tamko la Serikali juu ya njia mbadala za kupambana katika kipindi hiki cha upungufu wa huduma ya Maji kwa kuruhusu wenye visima binafsi kuwahudumia Wananchi. 

Akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe Godwin Gondwe na Afisa Mtendaji Mkuu-DAWASA, Cyprian Luhemeja, Mhe Aweso amesema Serikali ipo bega kwa bega na Wananchi wa Jiji la Dar es salaam na Pwani katika kipindi hiki na kuitaka Mamlaka ya Maji (DAWASA) kuhakikisha migao ya maji iliyowekwa kufuatwa bila ubabaishaji ili kutoa haki kwa kila mwananchi kuhifadhi maji ya kutosha wakati huu.

"Niwaagize DAWASA kuhakikisha ratiba ya mgao inasimamiwa na kufuatwa kikamilifu kama ilivyopangwa.

Pasitokee janja janja yoyote itakayosababisha lawama au upendeleo. 

Niseme kuwa Serikali imeruhusu matumizi ya maji ya visima binafsi na vya umma ili vitumiwe na kuendelea kutoa huduma kwa Wananchi bila kikwazo chochote hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo" alisisitiza Mhe Aweso

"Wenye visima binafsi toeni huduma sasa ili wananchi wasiteseke na huduma hii. 

Wizara inayo mipango ya muda mfupi ikiwemo  kuanza kutumia maji ya mradi wa Maji Kigamboni ambao utawashwa Oktoba 30. Amesema  mradi unatarajiea kuzalisha takriban lita milioni 70 za maji ambazo zitasambazwa Kigamboni na  maeneo ya katikati ya jiji" ameongezea Mhe Aweso

Waziri Aweso ameongeza kuwa hivi karibuni utiaji saini wa kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa Maji Kidunda utafanyika mwezi Novemba mwaka huu na kushuhudiwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassani. 

Mradi wa Kidunda ni suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji ghafi katika Mto Ruvu kwani litatumika kukusanya maji wakati wa mvua na maji hayo yatatumika nyakati za kiangazi.

Share To:

Post A Comment: