Naibu Waziri wa Kilimo Mh.Anthony Mavunde ametoa rai kwa mamlaka za upangaji wa matumizi ardhi nchini kubainisha maeneo ya kilimo na kuwapanga vizuri wakulima ili kupunguza migogoro ya ardhi inayosababishwa na mahitaji ya shughuli za kilimo na hivyo kupelekea uvamizi katika baadhi ya maeneo ambayo yanalindwa kisheria.

Naibu Waziri Mavunde ameyazungumza jana Katika mkutano wa Wananchi wa Kijiji cha Kibengula,Wilayani Mufindi-Mkoani Iringa wakati wa ziara ya Kamati ya mawaziri 8 wa kisekta ya utatuzi wa Migogoro ya ardhi ya Vijiji 975 nchini.

“Kilimo ni shughuli ya uzalishaji mali ambayo hitaji lake kubwa ni ardhi,na ni dhahiri kwamba asilimia kubwa ya watanzania wanakifanya kilimo kama shughuli yao kuu ya kiuchumi.

Nitoe rai kwa mamlaka za upangaji matumizi bora ya ardhi nchini kuhakikisha wanaweka kipaumbele katika kubainisha maeneo ya kilimo na kuwapanga vizuri wakulima ili shughuli za kilimo zifanyike katika maeneo yaliyotambuliwa rasmi.

Utambuzi na upangaji huu utasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi hasa kwa wakulima na wafugaji,lakini pia itasaidia kupunguza uvamizi katika maeneo ya hifadhi za misitu kama ambavyo inatokea hivi sasa.

Serikali inaendelea na zoezi la kupima Afya ya Udongo nchi nzima ili kusaidia kuwapa wakulima taarifa sahihi ya ikolojia ya maeneo yao ya kilimo juu ya aina ya mazao ya kupanda na aina ya mbolea za kutumia”Alisema Mavunde

Ziara hiyo ya Kamati ya mawaziri 8 wa kisekta ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Vijiji 975 inaendelea leo na ziara yake katika mkoa wa Njombe na baadaye Ruvuma.






Share To:

Post A Comment: