MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi amewataka wananchi hususani wa mkoa wa Arusha kuacha matumizi makubwa ya chumvi inayosababisha shinikizo la juu la damu ambalo moja ya madhara yake ni kutanuka kwa moyo.

Prof. Janabi ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ametoa wito huo leo tarehe 29/09/2022 wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Arusha Lutheran Medica Centre.

Alisema watu wengi wanapenda kutumia chumvi nyingi katika chakula hasa chumvi mbichi ambayo inaongezwa baada ya chakula kuiva, unywaji wa juisi za kusindika au kuongeza sukari pindi wanapotengeneza juice pamoja na kula kwa wingi vyakula vyenye wanga vitu ambavyo ni hatari kwa afya ya moyo.

Mkurugenzi huyo mtendaji alisema ukanda wa Arusha unawafugaji wengi na nyama inapatikana kirahisi kutokana na hali hii watu wengi wanapenda kula nyama choma ambayo asilimia kubwa ya chumvi inayotumika ni mbichi kitu ambacho kitasababisha changamoto ya afya kwa siku za usoni.

“Magonjwa ya kisukari na Shinikizo la damu yanatokana na mtindo wetu wa maisha hivyo tupunguze sana ulaji wa chumvi na matumizi makubwa ya sukari kwani asilimia 32 ya vifo vinatokana na magonjwa yasioambukiza hususani moyo na matibabu yake ni gharama kubwa”,.

“Ili kukabiliana na magonjwa ya moyo wananchi tujitahidi kufuata mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kuacha uvutaji wa sigara, kuacha unywaji wa pombe uliokithiri, kufanya mazoezi ikiwa ni pamoja na kutembea hatua elfu 10 kwa siku pamoja na kula vyakula bora”, alisema Prof. Janabi.

Aidha Prof. Janabi aliwataka wananchi kukata bima za Afya kwani gharama za matibabu zimekuwa zikiongezeka kadri siku zinavyokwenda lakini kama mtu atakuwa na bima ya afya itamsaidia kulipia gharama za matibabu pindi atakapoumwa.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Elisha Twisa aliwashukuru wataalamu ya JKCI ambao wako katika hospitali hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani.

“Tunawashukuru wenzetu wa JKCI ambao wametuletea huduma za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo katika mkoa wetu wa Arusha, tutazidi kushirikiana nao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii mara kwa mara”, alisema Twisa.

Mkurugenzi huyo mtendaji wa ALMC alisema hospital hiyo ipo mbioni kuanzisha kitengo cha matibabu ya moyo ili kuwasaidia wananchi waweze kupata huduma hiyo karibu zaidi.

Mmoja wa wananchi aliyepata huduma za upimaji na matibabu Kulwa Mayombi alisema yeye pamoja na wenzake wamefurahia kupata huduma hiyo sanjari na elimu ya afya itakayowasaidia kuondokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.

Katika kuadhimisha siku ya moyo dunia ambayo kauli mbiu yake ni “fanya uamuzi sahihi kuhusu moyo wako” wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano iliyoanza tarehe 26 hadi 30 mwezi huu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani.
Share To:

Post A Comment: