Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amempa saa 24 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini, Khalfani Magani kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa madai ya kuficha fedha za mfadhili za ujenzi wa shule.

Agizo hilo amelitoa jana Alhamisi Septemba Mosi 2022 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mgwashi iliyopo wilayani Korogwe, akimtaka kiongozi huyo ajieleze kwa nini asiondolewe kwenye nafasi yake hiyo.

Mgumba amesema kuwa ameamua kutoa maagizo hayo baada ya mkurugenzi huyo kuchelewesha ujenzi wa shule ya sekondari Mgwashi uliokuwa ukamilike Juni mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema shule hiyo ilipatiwa mgao na Serikali wa Sh600 milioni ambapo awali walipokea Sh470 milioni huku mfadhili alishatoa zaidi ya Sh100 milioni kwaajili ya ujenzi huo lakini Mkurugenzi huyo hakutaka kueleza taarifa hiyo ya Mfadhili kwenye kikao chochote.

"Umeletewa fedha mwezi wa 12 (Desemba) na huu mradi ulitakiwa ukamilike mwezi wa nne (Aprili), kuna watu walikuwa na nia ovu ya kumchonganisha Rais (Samia Suluhu Hassan) na wananchi wa Mgwashi hatutawavumilia na hawana nafasi kwenye utawala huu,"  amesisitiza Mgumba.


Mgumba amesema miradi ikicheleweshwa hauna ufanisi wala gharama halisi ya fedha   na pia inakuwa imecheleweshwa huduma kwa wananchi.

Mbali na mkurugenzi huyo kutakiwa kujieleza lakini pia aliagizwa kuanza kulipwa a fidia leo kwa wananchi 48 waliokuwa wanalima kwenye eneo hilo ambalo linajengwa shule hiyo ya sekondari.

Kwa upande wao wananchi wamesema kuwa kukosekana Kwa shule ya sekondari kulikuwa kunasababisha utoro wanafunzi kwani shule waliyokuwa wanategemea ilikuwa na umbali wa kilometa 5 hadi 10.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huyo aliwataka wananchi waanze kuchimba msingi kwaajili ya kuanza ujenzi wa shule hiyo ili watoto wa kata hiyo waondokane na changamoto hiyo sugu.

Ameongeza kuwa, “Mkurugenzi nataka ujieleze ndani ya masa 24 kwanini umechelewesha mradi na kwamba majibu yake kama yatanidhisha ndiyo nitamshauri Rais au Waziri hatua gani za kufanya na tabia ya kuchelewesha mradi iwe mwanzo na mwisho.”


H.T : Mwananchi

Share To:

Post A Comment: