Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewagiza viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Karatu kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo ili iweze kukamilika kwa wakati na wananchi waanze kupata huduma.

Mongella ametoa maagizo hayo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.

Katika ziara yake Mhe Mongella amesisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati kutasaidia kuongeza thamani ya miradi hiyo.

Akiwa katika  mradi wa Kilimo cha Vitunguu katika Kata ya Mang'ola, Mongella amewaahidi wakulima hao kuwasaidia kuwatafutia masoko ya Vitunguu ya uhakika ili kilimo hicho kiwezu kuwa na tija na manufaa kwa wakulima wenyewe na Taifa kwa ujumla.

Aidha amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili wananchi wake waweze kupata huduma bora na kwa ukaribi zaidi ambapo amewataka wananchi kuithamini na kuitunza miradi hiyo kwani ni kwaajili yao ili waweze kupata huduma muhimu kwa ukaribu zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Holace Kolimba amesema wao kama Wilaya wanashirikiania kwa ukaribu sana na viongozi wa Halmashauri ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa haraka kama ilivyopangwa.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu  Karia Rajabu amesema watayasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili Halmashauri hiyo iweze kukamilisha miradi yote ya maendeleo kwa wakati.

Katika ziara hiyo Mhe. Mongella ameweza kukagua ujenzi wa majengo katika shule ya Sekondari Ayalabe yaliyogharimu Milioni 470 kwa awamu ya kwanza, Ujenzi wa majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Karatu yenye thamani ya fedha bilioni 2.4, upandaji na uvunaji wa Vitunguu katika Shamba la Mang'ora.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: