ZIARA ya Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, ya kata kwa kata aliyoipa jina la Huduma Jimboni Julai 21, imeingia siku ya nne ambapo ametembelea Kata ya Issuna Kijiji cha Ng’ongosoro na Kitongoji cha Manjaru.

Katika ziara hiyo Mtaturu,amekagua miradi ya maendeleo na kuwapa mrejesho wa Bajeti ya Serikali iliyopitishwa mwishoni mwa mwezi Juni 2022.

Akiwa katika ziara hiyo Mtaturu,amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka Sh. Milioni 64 kwa ajili ya kufungua barabara ya Nkuhi – Manjaru yenye kilomita 21 na kuweka madaraja mawili.

“Rais Samia pia ametoa Sh Milioni 35 kwa ajili ya kuweka madaraja na kupandisha matuta katika barabara ya Issuna – Ng’ongosoro – Ilolo,niwahakikishie kuwa Rais wetu ana dhamira ya dhati ya kutuletea fedha ili miradi ya maendeleo itekelezwe,”amesema.

Amewahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi Agosti 23,2022,ili nchi ijue idadi ya watu waliopo.

Aidha,katika ziara hiyo Mtaturu alipita katika shule ya msingi Inang'ana na kuwapongeza walimu na wazazi kwa kushirikiana na kusimamia taaluma.

“Walimu wangu najua mnafanya kazi kubwa na nzuri sana katika kuwalea watoto wetu kitaaluma,kazi yenu naithamini sana,na katika vipaumbele vyangu mimi kama mbunge sekta ya elimu ni mojawapo,nimepita hapa kuwasalimu,kuwashukuru na kuwaletea kidogo nilichonacho kiwe kama motisha kwenu,”amesema.

Akiwa shuleni hapo ametoa Kilo 100 za mchele,ametoa Sh 150,000 kwa walimu watatu wanaojitolea na Sh 100,000 kwa ajili ya kununua sukari kama motisha kwa kazi nzuri wanayaoifanya kuwahudumia wanafunzi kwa moyo wa kujitolea na mipira miwili kwa ajili ya mpira wa pete na wa miguu ili kuwafanya vijanna waepukane na makundi mabaya na kujenga undugu na umoja.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Issuna Stephano Misai amemshukuru mbunge kwa kuendelea kuwasemea bungeni bila kuchoka ili kuwaletea maendeleo.

"Ahsante sana mbunge wetu Mtaturu,kata ya Issuna inashuhudia miradi mingi ikitekelezwa katika kipindi hiki,na tunajua ni jitihada zako za kutusemea,mfano Zahanati ya Isuna imekalimika na tumepewa mgao wa watumishi wawili,na sasa tunasubiri mgao wa dawa ili huduma zianze,"amesema.

Amesema kupitia mfuko wa jimbo wamepelekewa Sh Milioni 4 ili kujenga madarasa ya shule ya msingi Ng'ongosoro,lakini kubwa ni hii barabara ya Nkuhi -Manjaru kufunguliwa kwani ilikuwa ni changamoto kubwa sana tangu nchi imeumbwa hapakuwa na barabara.

Ziara hiyo ina lengo la kufika katika kata na vijiji vyote vilivyopo katika Jimbo hilo,hakika hakuna jiwe ambalo halitageuzwa.

#SENSA 2022, Jitokeze, Jiandae kuhesabiwa ewe mwana Singida Mashariki.Share To:

Post A Comment: