Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona |
*****************
Muheza, Tanga
Serikali
imesema watu waliopewa mashamba katika Shamba la Mkonge la Kibaranga
(Kibaranga Sisal Estate) lililoko Muheza mkoani Tanga na
hawajayaendeleza au wameyaendeleza kwa mazao mengine watanyang’anywa.
Shamba
hilo lenye Hekta 5,600 ambalo linamilikiwa na Bodi ya Mkonge na
kusimamiwa na Amcos ya Kibaranga baada ya serikali kulirudisha kutoka
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ambao walionyesha kusua sua katika
uendelezaji wa shamba hilo.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema
hayo jana katika kikao na viongozi wa Chama cha Ushirika wa Mazao na
Masoko (Amcos) cha Kibaranga na wa kijiji ambapo pamoja na mambo mengine
wananchi walitaka kujua utaratibu wa kuendeleza maeneo hayo kwa ujenzi
wa nyumba.
Hoja
hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kibaranga Amcos, Paulo Haule ambaye
alisema amepata maombi ya wananchi wananchi katika eneo hilo wakitaka
kujenga makazi ndani na pembezoni mwa shamba hilo.
Akijibu
hoja hiyo, Kambona alisema shamba hilo liligawiwa eka tatu kwa kila
mkulima ili walime na kuendeleza zao la mkonge lakini wengine wamefanya
kilimo cha mazao mengine kinyume na makubaliano.
“Labda
niwakumbushe tu hili shamba linaitwa Kibaranga Sisal Estate, ni shamba
la mkonge si shamba la michungwa. Lakini pia niwaambie wakazi wa Muheza
popote walipo wajue kuwa hawajapewa hizi ardhi ili wajenge nyumba,
walipewa zile eka tatu tatu ekari moja ulime mkonge halafu ndiyo upande
mazao yako mengine.
“Tunafahamu
Mheshimiwa Waziri Mkuu amefika hapa mara tatu na mara zote amesisitiza
suala la uongezaji wa uzalishaji na ndiyo sababu ya shamba hili
kurudishwa Bodi ya Mkonge baada ya kuonekana kuwa tangu imekaa
halmashauri hakuna uendelezaji wa kilimo cha mkonge uliofanyika kuanzia
shamba lenyewe na mashine ambayo inatakiwa ifufuliwe ili ianze kuchakata
mkonge.
“Kwa
hiyo serikali imesema shamba lirudi Bodi ya Mkonge na bodi iratibu
shughuli za uendelezaji wa hili shamba,” alisema Kambona.
Alisema
Bodi ya Mkonge ikishirikiana na Amcos ya Kibaranga ambayo ni moja ya
Amcos changa lakini zinakuja vizuri kwa sababu ya umadhubuti wa uongozi
ambapo wanashirikiana nao vizuri wakisaidia ugawaji kwa maana ya kuleta
hali ya utulivu kwenye shamba hilo na kuhakikisha wanaratibu masoko ya
mkonge kwa wale waliofikia hatua ya kuvuna.
“Sasa
niwaambie tu wananchi wa Kibaranga, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya
Muheza, Halima Bulembo wakati amekuja tu mwaka jana alifanya kikao hapa
na akarejea maagizo ya Waziri Mkuu kwamba waliopewa mashamba hapa walime
mkonge, hili ni shamba la mkonge kwa hiyo walime mkonge.
“Kama
umepewa shamba na hujaliendeleza, shamba hilo utanyang’anywa na kupewa
mtu mwingine ambaye yuko tayari kulima mkonge. Kwa hiyo isikupe sifa
kwamba mimi ninayo hati halafu una miaka sita tangu upewe hilo shamba
hujaendeleza kwa kilimo cha mkonge,” alisema.
Aidha,
Kambona alisema Bodi itatoa tarehe ambayo ikivuka hiyo tarehe mashamba
hayo yote yataanza kugawiwa upya kwani hawataki kuona mapori wanataka
kuona mkonge ukiwa umeshamiri.
Alisema
shamba hilo ni kubwa ambapo likipandwa mkonge tayari linakuwa
limeshafikia lengo la serikali kwa asilimia kubwa kwani litakuwa
limeongeza uzalishaji kuelekea tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.
“Kwa
hiyo wananchi watambue hivyo na serikali iko makini sana ni kweli wale
ambao hawataendeleza mashamba yao kwa kilimo cha mkonge
tutawanyang’anya, umepanda machungwa ndani ya shamba la Kibaranga
tutakunyang’anya hilo eneo tumpe mtu mwingine,” alisema.
Pamoja
na mambo mengine, Kambona alisema Wilaya ya Muheza ina ardhi nzuri kwa
kilimo cha machungwa nje ya shamba la Kibaranga na Shamba la Kibaranga
limetengwa kwa ajili ya kilimo cha mkonge tu na mazao mengine ambayo ni
ya muda mfupi kama mahindi au alizeti ni sawa kulima ndani ya mkonge.
Alisema
Bodi ya Mkonge ndiyo itaratibu ni namna gani ya kuendeleza shamba hilo
na eneo na watu wote watazingatia masharti ambayo yatatolewa na Bodi
kwenye namna ya uendelezaji wa shamba hilo.
“Sasa
watakaochukua hatua za kufanya makubaliano au mauziano huko nje bila
kufuata utaratibu ambao utawekwa na Bodi ya Mkonge wasishangae kuona
watapoteza hizo ardhi kwa sababu Bodi itawanyang’anya na hatutambui hayo
mauziano tutawapa watu ambao wamefuata utaratibu wa kumilikishwa haya
mashamba,” alisema.
Alisema
bodi inataka watu wajue kilimo cha mkonge ni kilimo makini na kilimo
ukikizingatia kitabadilisha hali ya maisha kwa haraka sana.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao na Masoko wa Bodi ya
Mkonge, Olivo Mtung’e, alisema kwa sasa suala la kujenga makazi ndani ya
shamba hilo haliwezekani kwani litaleta mgogoro kutokana na ukweli
kwamba baadhi ya watu watauza maeneo yao na baada ya muda mfupi patakuwa
makazi ya kudumu.
“Tukisema
tujenge huu mgogoro hautakuwa mdogo kwa sababu sisi Waafrika familia
zetu huwa zinaongezeka tu ukijenga wewe leo kesho mtoto wako pia atataka
kujenga kwa ajili ya makazi, kwa hiyo maana ya kuwa shamba la mkonge
itaondoka, kwa hiyo suala la kujenga makazi ya kudumu kwa sasa
hapana,”alisema.
Post A Comment: