NA EMMANUEL MBATILO, DODOMA
Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NCSS), unaoratibiwa na shirika la HakiElimu, umetoa wito kwa wadau kuunga mkono jitihada za pamoja za kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili.
Wito huo umetolewa Desemba 16, 2025 jijini Dodoma wakati wa mkutano wa kufunga mwaka na kufanya tathmini ya mpango kazi wa mwaka mzima.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Idara ya Utafiti, Ubunifu na Uchambuzi wa Sera – HakiElimu, Makumba Mwemezi, amesema mkutano huo umezikutanisha taasisi zinazotekeleza mpango wa Shule Salama kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu mpya za kuhakikisha usalama wa mtoto.
“Lengo letu ni kujenga sauti ya pamoja ya kukemea, kupinga na kutoa ushauri kuhusu masuala ya ulinzi wa mtoto, ikiwemo kupinga adhabu ya viboko,” amesema Mwemezi.
Ameongeza kuwa hadi sasa umoja huo una wanachama 24 na unaendelea kupokea wanachama wapya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya KAYA, Pili Anna Ngome, amesema mkutano huo umewezesha kufanya tathmini ya pamoja ili kubaini changamoto na kuandaa mikakati bora ya kusonga mbele.
Naye Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Haki za Watoto Tanzania (TCRF) Bw. Ombeni Kimaro, amesema kikao hicho kimelenga kutathmini mafanikio ya awali na kuandaa mpango kazi wa mwaka ujao, kwa kuzingatia changamoto zinazoanzia nyumbani hadi shuleni.
Aidha, Mratibu wa ZAPHA+, Mussa Tanu Juma, amesema umoja huo kwa kushirikiana na serikali umechangia kusukuma masuala ya ulinzi wa mtoto kuingizwa kwenye mitaala, hususan yanayohusu ukatili wa kijinsia na adhabu ya viboko.
Kwa upande wake, Amina Ally Mtengeti kutoka MyLegacy amesema umoja huo umeondoa changamoto ya taasisi kufanya kazi kivyake, na badala yake umejenga nguvu ya pamoja katika kushawishi mabadiliko ya kisera na kimfumo kwa ustawi wa mtoto.
UMOJA wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NCSS) unaundwa na taasisi za Kaya Foundation, HakiElimu, Save the Children, SAWA Morogoro, MTWANGONET, Msichana Initiative, ZAFELA, TAMWA, ZALHO, WILDAF, MyLegacy, Child Dignity Forum, Child Support Tanzania, HGWT, ZCRF, TCRF, ZAPHA+, Children in Cross Fire, Amani Girls Organization, Women Fund Tanzania Trust, Shule Direct, CAMFED, Plan International and TENMET
























Post A Comment: