Mratibu wa Utafiti wa zao la Korosho Kitaifa kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, Dk. Geradina Mzena akizunguza katika hafla fupi ya kumpokea Mtaalam wa Kilimo Bora cha zao la Korosho iliyofanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni ikiwa ni utekelezaji wa  agizo la Waziri wa Kilimo la kuitaka TARI kumpeleka mtaalam huyo wilayani humo ili kwenda kuwasaidia wakulima wa zao hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Melkzedeki Humbe akiishukuru Serikali na TARI kwa hatua ya kumpeleka mtaalam huyo ambaye walikuwa wakimuhitaji kwa siku nyingi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo wilayani humo.
Mtaalam huyo, George Lucas (kushoto) akizungumza wakati akijitambulisha kwenye hafla hiyo.
Hafla ya kumpokea mtaalam huyo ikiendelea. Kulia ni Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Wilaya ya Manyoni, Ray Mtangi na wa pili kushoto ni Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika  wa Wilaya ya Manyoni.Fadhili Chimsala.

Hafla ya mapokezi ikiendelea. Aliyeipa kamera mgongo ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa.
 


Na Dotto Mwaibale, Manyoni.


KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele kilichopo mkoani Mtwara kinachojishughulisha na majukumu ya kufanya utafiti wa mazao makubwa kitaifa ya korosho na mbegu za mafuta ambayo ndani yake kuna ufuta na karanga kimetekeleza agizo la Waziri wa Kilimo kwa kumpeleka Mtaalam wa Kilimo Bora cha zao la Korosho wilayani Manyoni mkoani Singida ili kuwasaidia wakulima.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumpokea mtaalam huyo aitwaye George Lucas iliyofanyika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani hapa jana, Mratibu wa Utafiti wa zao la Korosho Kitaifa kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI, Naliendele, Dk. Geradina Mzena alisema wao kama Taasisi wametekeleza agizo la Waziri wa Kilimo Hussein Bashe la kuwataka kumpeleka mtaalam wa zao hilo wilayani humo ili kwenda kuwasaidia wakulima wa zao hilo.

"Tumetekeleza agizo la Waziri la kumleta wilayani hapa mtaalam huyu ambaye atakuwa akiwasidia wakulima ili waweze kulima kilimo cha zao la korosho chenye tija kwa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na wakulima na si kwa Manyoni pekee bali na kwa wakulima wa mikoa mingine ya jirani" alisema Dk.Mzena.

Dk.Mzena alisema lengo la TARI nikuona wakulima wanalima kilimo chenye tija cha zao hilo na wananufaika nacho na wanainuka kiuchumi na Serikali inapata mapato.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Melkzedeki Humbe aliishukuru Serikali na TARI kwa hatua hiyo ya kumpeleka mtaalam huyo ambaye walikuwa wakimuhitaji kwa siku nyingi kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo wilayani humo.

"Tunashukuru sana kwa ujio wa mtalaam wa zao la korosho tunaamini atasaidia kuinua kilimo cha korosho wilayani kwetu na ujio wake ni neema kwetu ukizingatia kuwa zao la korosho ni la kimkakati na tegemeo kwa kuinua uchumi wa wilaya yetu na Taifa kwa ujumla na tutampa ushiriano mkubwa" alisema Humbe.

Hafla ya kumpokea mtaalaam huyo ilihudhuriwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Rahabu Mwagisa, wataalamu wa kilimo wilayani humo akiwepo na Kaimu Meneja wa Bodi ya Korosho Wilaya ya Manyoni, Ray Mtangi.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: