Na Richard Bagolele-Chato


Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Rosemary Senyamule amesema kutokana na fursa nyingi zilizopo wilayani Chato  na miradi mingi mizuri inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya sita mara tu baada ya  kukamilika kwa miradi hiyo itatimiza malengo ya wakazi wa Chato na watanzania kwa ujumla.


Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti 

na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) za mwaka 2020/2021 kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri.


Mkuu wa Mkoa amesema kutokana na Wilaya ya Chato kuwa na uwanja wa ndege, wageni wengi watafika wilayani hapa kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ile ya utalii, huduma za Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Chato, mnada wa Ng'ombe wa Buzirayombo na miradi mingine mikubwa iliyopo hapa, hivyo amewaasa  wananchi kuendelea kutoa ushiriakiano kwa serikali ili kuweza kufikia malengo pamoja na kukamilisha miradi hiyo na mingine mipya.


"Najua Wilaya ya Chato inazo ndoto kubwa na nyingi sana, kiasi chake zimeanza kutimia, ndoto kubwa ni kuwa wilaya ya utalii na niwahakikishie ndoto hizo zitatimia" amesema Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Kwa upande wa hoja za CAG Mkuu wa Mkoa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuendelea kupata hati safi kwa muda miaka sita mfululizo ambapo ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuhakikisha hoja zote za CAG zinajibiwa na kufutwa kwa wakati.


"zipo hoja zinazofutwa na  Halmashauri, zinazofutwa ngazi ya Mkoa, na zingine kupitia kwa waziri, kaeni vikao mfute hoja hizi" alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Kwa upande wake Mkaguzi mkuu wa nje wa Mkoa wa Geita ACPA Richson Ringo ameshauri Halmashauri kuwajengea uwezo wahasibu, maafisa manunuzi na wale wote wanaohusika na uandaaji wa taarifa za fedha ili waweze kupatiwa mafunzo maalumu na ya kina ili kuepukana hoja za ukaguzi.


Mkuu wa Wilaya ya Chato  mhe. Martha Mkupasi amesema pamoja na Wilaya ya Chato kuwa na miradi ni vyema kuimaraisha usimamizi wa miradi hiyo kwa umakini mkubwa hasa kupitia kitengo cha Manunuzi kwani hoja nyingi zinasababishwa na   watumishi wenyewe. Amewaomba watumishi wa Halmashauri kusimamia kwa umakini ili kuweza kuzuia hoja mpya pamoja na kufunga hoja zilizopo.


Makamu Mwenyekiti wa Halamshauri Mhe. Fortunatus Jangole amesema Halmashauri itachukua hatua kwa wale wote waliosababisha hoja hizo ambapo amesema ni wakati sasa wataalamu wa Halmashauri kuhakikisha inafuta hoja ambazo zinawezekana kufutwa ili kupunguza idadi ya hoja za CAG.

Share To:

Post A Comment: