Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro (kushoto) akifurahia ramani ya Jengo la kuratibu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIWOHEDE, Mama Justa Mwaituka.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Jerry Muro (kushoto) akionesha kwa Waandishi wa habari muonekano wa Jengo litakalojengwa wilayani mwake kwa ajili ya kuratibu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake. Kushoto ni Mkurugenzi.
Pichani ni mtoto ambaye amepitia ukatili wa hali ya juu kwa watoto. Inaaminika kuwa asilimia 90 ya Vitendo vya Ukatili dhidi ya watoto husababishwa na wanafamilia.

Huyu ni mmoja wa watoto wanaopitia Ukatili dhidi ya watoto.


 

Na Abby Nkungu, Singida

 

WILAYA ya Ikungi mkoani Singida inakusudia kutumia zaidi ya shilingi milioni 110 kwa ajili ya  utekekezaji wa shughuli za mradi wa ujenzi wa kituo maalum cha kupinga vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia kwa  watoto  na wanawake katika  kipindi cha mwaka ujao wa fedha wa 2023/24.

Mkuu wa Wilaya hiyo Jerry Muro alisema kuwa ujenzi wa  kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa kuhusu Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT - MMMAM) inayoendelea hadi 2026.

Alisema kuwa lengo la hatua hiyo ni kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu, jumla ya watoto 36 wenye umri wa chini ya miaka minane (0 - 8), wamefanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia.

DC Muro alifafanua kuwa watoto hao wamefanyiwa ukatili wa kingono, kimwili, kihisia au utekelezaji hivyo kuwasababishia madhara ya kisaikolojia, magonjwa, ulemavu, kupoteza ndoto zao na haki ya elimu na kuleta ongezeko la watoto waishio mazingira magumu na hatarishi.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, kesi 9 zipo mahakamani, moja ilifungwa kituo cha polisi, nyingine iko rufaa Ustawi wa Jamii na zilizobaki watuhumiwa hawakuweza kupatikana. 

Alisema kuwa pamoja na shughuli hiyo kuwemo kwenye utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa, mradi huo mkubwa wa aina yake umetokana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayoelekeza kila wilaya kukomesha matukio na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake.

 "Mradi huu unafadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali la KIWOHEDE. Mimi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mama Justa Mwaituka tumekamilisha mazungumzo na kwa pamoja tumekubaliana ujenzi wa jengo litakaloitwa MKONO SHUFAA na miundombinu muhimu, uanze mara moja. Jengo hilo litajengwa katika hospitali ya Wilaya yetu" alieleza DC Muro.

Alisema kuwa  pamoja na ujenzi wa kituo  hicho,  pia  wanaendelea kutoa elimu kwenye Jamii na shuleni juu ya namna ya kupinga ukatili wa kijinsia, kuanzisha  kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto kwa kushirikisha jamii na wadau mbalimbali na kuendeleza utoaji wa elimu ya Malezi na Makuzi kwa wazazi na Jamii kwa kushirikisha Jeshi la Polisi kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE, Justa Mwaituka alieleza kuvutiwa na jinsi ambavyo wilaya hiyo inapambana katika kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii na kuahidi kuendelea kutoa misaada mbalimbali ya hali na mali ili kutokomeza vitendo hivyo.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wanasema pamoja na hatua hizo bado kuna haja ya kutoa   elimu zaidi kwa jamii juu ya umuhimu wa kuzuia  na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

“Jamii yetu bado haina elimu ya kutosha. Unakuta mtu mtoto wake amefanyiwa ukatili wa kingono kwa kulawitiwa au kubakwa lakini wanamaliza suala hilo kifamilia. Hii haisaidii kukomessha vitendo hivyo” alieleza Patrick Mdachi Ofisa Maendeleo ya Jamii mstaafu na kuungwa  mkono na Rehema Daniel aliyetaka viongozi wa Mitaa na Vijiji kuacha kumaliza masuala hayo ngazi za chini bali wayafikishe kwenye vyombo vya sheria.

Walisema kuwa iwapo hatua za kisheria zitachukuliwa kikamilifu dhidi ya wahusika wa vitendo  vya ukatili kijinsia kwa watoto,  itasadia kutoa funzo na kuogofya watu wengine wenye nia ovu katika jamii yote.

Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk. Suleiman Muttani anasema kuwa ukatili wa kijinsia kwa watoto umekuwa  na madhara makubwa kwa kundi  hilo na kuleta athari za kiafya na kisaikosojia kwa muda mrefu na mfupi.

Dk. Muttani ameshauri kuwepo mikakati madhubuti kwa ajili ya kudhibiti vitendo hivyo katika jamii kwa kuwa baadhi yake vina athari kubwa kwa afya ya mtoto hata baada ya mtoto huyo kuwa mtu mzima. 


 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: