Wananchi wa kata ya Dumbeta Halmashauri ya wilaya ya Hanang wameomba kupatiwa huduma ya maji na nishati ya umeme kwenye kijiji chao wakidai kuwa kukosekana kwa huduma hiyo imesababisha kuchelewesha maendeleo kijijni hapo.

Wamesema mbali na kukosekana kwa maji na umeme lakini pia bara bara imekuwa kikwazo kwao kuweza kusafirisha mazao yao na kwenda kupata huduma zingine ikiwemo za afya.

Wametoa ombi hilo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Hanang' Mhandisi Samwel Hhayuma alipofanya ziara katika kata hiyo kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo na kuzipatia ufumbuzi.

Akijiwajibu wananchi hao, Mheshimiwa Hhayuma amewaagiza TANESCO kuunganisha huduma ya umeme haraka katika kata hiyo ili kuchochea kasi ya maendeleo na kuvutia wawekezaji kwani katika kata hiyo hakuna eneo lolote lenye huduma ya umeme.

Aidha kwa upande mwingine Mbunge huyo akizungumza kuhusu changamoto ya ukosefu wa dawa katika hospitali ya wilaya hiyo Tumaini,amesema suala hilo ataliwasilisha katika baraza la Madiwani.

Mbunge Hhayuma katika ziara hiyo aliambatana na viongozi wa chama na wataalamu wa idara mbalimbali.


Share To:

Post A Comment: