Waziri  wa Elimu, Sayansi ya Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo, Prof. Adolf Mkenda ameshuhudia mechi ya fainali ya kombe la Rombo yaliyojulikana kama Mkenda Cup 2022, ambapo timu ya  Motamburu Kitendeni iliibuka na ushindi.


Katika mechi ya fainali iliyochezwa April 24, ilizikutanisha timu mbili za Motamburu Kitendeni na Ubetu Kahe, ambazo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 hadi dakika ya 90 na kwenda kwenye  mikwaju ya penalti ambayo iliipa ushindi Motamburu Kitendeni kwa kushinda penalti  6 kwa 5 dhidi ya mpinzani wake.


Mshindi wa kwanza katika mchezo wa fainali ya Mkenda cup 2022 aliibuka na kitita cha Shilingi milioni mbili pamoja na kombe, mshindi wa pili akiibuka na Sh. milioni moja huku mshindi wa tatu ambayo ni timu ya Nanjara ikiibuka na Sh. 500,000 ambapo mfungaji bora aliondoka na kiatu cha dhahabu huku  kipa bora akijishindia jezi, gloves na soksi.


Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi hao, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe.David Silinde ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye fainali ya mashindano hayo alipongeza washiriki wa mashindano hayo kwa vipaji vikubwa walivyovionesha huku akieleza jukumu lililobaki kuwa ni la Serikali kuendeleza vipaji hivyo.


Alisema mpango wa Serikali ni kujenga shule za vipaji kwenye kanda nane nchini ambazo zitasaidia kuibua vipaji ambapo kwa kupitia mashindano kama ya Mkenda Cup yatairahisishia Serikali kutambua vipaji vilivyopo kwa urahisi.


 “Nimpongeze Mbunge wa Rombo, Prof. Mkenda  ambaye ndiye mdhamini wa mashindano haya, kazi aliyoifanya kuunganisha vijana kwa timu 63 kwa zaidi ya miezi minne siyo rahisi, na vijana hawajamuangusha wameonesha kuwa Rombo kuna vipaji vikubwa na wapo imara,” alisema Mhe. Silinde.


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Rombo, Mhe. Prof. Mkenda alisema ataendelea kudhamini ligi hiyo ya mpira wa miguu kwa mwaka 2023 ambapo kwa sasa wataendelea kucheza mechi za kirafiki kwa kila Kata ambazo kila mchezo utakuwa na zawadi.


“Baada ya fainali hii tutaanza kucheza michezo ya kirafiki mpaka mwezi Desemba ambayo itaitwa Samia Friendship Tournament kwa heshima ya Rais wetu na kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya kwa Jimbo la Rombo,” alisema Prof. Mkenda.


Share To:

Post A Comment: