Na Joachim Nyambo,Mbarali.


VITUO shikizi vilivyoboreshwa na fedha zilizotolewa na serikali kupitia Mpango wa Maendeleo  kwa Ustawi wa Taifa  na Mapambano dhidi ya Covid-19 havijaanza kufanya kazi wilayani Mbarali. 


Kutoanza kufanya kazi kwa vituo hivyo kunasababisha wanafunzi waliopaswa kuvitumia wakiwemo wale walioandikshwa kuanza darasa la awali na la kwanza kuendelea kusota kwa kutembea umbali mrefu kufuata masomo kwenye shule mama licaha ya umri wao mdogo. 


Hatari zaidi kwa watoto hawa uko katika kipindi hiki cha mvua nyingi ambapo kwa wilayani Mbarali ni jambo la kawaida mito kufurika na kukata mawasiliano ya barabara kati ya maeneo ya makazi ya watu na zilipo huduma za msingi hasa shule,nymba za ibada,vituo vya tiba na maeneo ya masoko. 


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza la Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali iliyo mlezi wa Mamlaka hiyo,Missana Kwangura alisema takribani vituo shikizi 13 wilayani hapa havijaanza kufanya kazi. 


Kwangura alisema miongoni mwa vituo ambavyo havijaanza kufanya kazi  kuwa ni pamoja na cha Mogelo,Nyamntowo na Mabambila ambavyo wanafunzi wake wakiwemo wa madarasa ya awali na la kwanza wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 hadi ziliko shule mama. 


Alisema kutoanza kufanya kazi kwa vituo hivyo kunatokana na uwepo wa changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vyoo kwakuwa bajeti ya fedha iliyoletwa awali na serikali Shilingi milioni 480 haikujumuisha ujenzi wa vyoo. 


Alisema tayari Halmashauri kwa makubaliano ya pamoja na Baraza la madiwani wametenga na kupeleka kiasi cha Shilingi milioni 118 kwaajili ya ujenzi wa vyoo kwenye vituo shikizi hivyo na hivyo kuanza kujengwa kwakuwa tayari wananchi walikuwa walikwisha chimba mashimo tang mwaka jana. 


“Vituo shikizi karibu vyote havikuwa na vyoo na hauwezi ukasajiri shule kama  haina choo.Nashukuru sana kamati ya fedha na baraza la madiwani waliruhusu kutoa shilingi milioni 118 kwaajili ya kwenda kujenga vyoo kwenye vituo shikizi vyote 13.” 


Alisema mara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo kamati maalumu itavitembelea vituo shikizi vyote na kufanya ukaguzi na mara tu baada ya kujiridhisha ruhusa itatolewa kwa vituo kuanza kufanya kazi. 


Alisema baada ya ruhusa kutolewa wanafunzi wote waliopaswa kuanza masomo yao kwenye vituo hivyo wataondolewa kwenye orodha ya shule mama wanazosoma hivi sasa zikiwa mbali na makazi yao na kuhamishika kwenye vituo husika ili waondokane na adha ya kutembea umbali kufuata masomo. 

“Vyoo vitakapokuwa vimekamilia jambo litakalofuata ni shule kuja kukaguliwa na wakaguzi wetu wa wilaya ambao kisha wataandika taarifa kwa maizingira hayo sasa ndiyo shule inaweza ikaanza.” 


“Lakini hata kama shule ikiwa haijakaguliwa vitakapokamilika vyoo wale watoto kwa sababu wanatembea umbali mrefu kama wale wa kituo shikizi cha Muungano wanatembea zaidi ya kilometa kumi..sasa we fikiria mtoto wa miaka sita au saba anatembea umbali wa kilomita kumi..ni mbali na anapita maporini na usalama wake ni mdogo sana..hawa tutaruhusu wananze kusoma ili mradi choo  kiwe kimekamilika ili kuwapungzia umbali na kuwaokoa na hatari.” 


Akizungumzia suala la uwepo wa walimu wenye kutosheleza mahitaji kwenye vituo shikizi hususani walio na ujuzi wa kufundisha masomo matatu muhimu kwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ya Kusoma,Kuandika na Kuhesabu maarufu kama K3,Kwangura aliwatoa hofu wazazi na walezi akisema wamejipanga kwa hilo. 


Alisema kwakuwa walimu wenye ujuzi huo wapo wa kutosha kwenye shule mama haitokuwa shida kuwagawanya na kuwapangia baadhi kwenye vituo shikizi ili elimu itakayotolewa kwenye vituo hivyo iwe sawa na ilivyo katika shule mama. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali,Twalib Lubandamo alisema madiwani waliona ulazima wa kutoa fedha kwaajili ya kujenga vyoo kutokana na kutambua umuhimu wa vituo shikizi hasa baada ya serikali kuu kutambua changamoto wanazopitia wanafunzi hususani walio na umri mdogo. 

Baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaopaswa kutumia vituo shikizi wilayani hapa waliomba halmashauri kuongeza kasi kwenye ujenzi wa vyoo ili wanafunzi waanze kunufaika na mpango wa serikali wa kuwapelekea karibu huduma ya elimu.

Share To:

Post A Comment: