Na WAF- DOM.


Wizara ya Afya imekabidhi mashine tano za kisasa za kuchanganya chumvi na madini joto kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI zilizotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition International kwa ajili ya kusimikwa katika Mikoa ya Tanga, Pwani na Mtwara itayosaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye kiwango cha kutosha cha madini joto nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Utafiti uliofanyika nchini mwaka 2019 ulibaini Tanzania inazalisha chumvi Tani 330,712 kwa mwaka na kati ya Chumvi hiyo Tani 141,228 ambapo ni sawa na asilimia 43 haiwekwi madini joto hivyo ujio wa mashine hizo utasaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye madini hayo.

Prof. Makubi amesema mashine hizo ambazo zimetengenezwa nchini na Wataalamu kutoka VETA zimeweza kugharimu kiasi cha shilingi milioni 55 huku gharama ya mashine moja ikigharamu kiasi cha shilingi milioni 11 na kusaidia kuokoa milioni 14 kwa kila mashine endapo zingeagizwa kutoka nje ya nchi.

“Mwaka 2018 Shirika la Nutrition International lilifadhili ununuzi wa mashine tatu zilizoagizwa kutoka Afrika Kusini kwa jumla ya Shilingi milioni 75 ambapo mashine moja iligharimu shilingi Milioni 25 na kusimikwa Halmashauri za Kilwa, Hanang na Meatu na zinaendelea kufanya kazi lakini safari hii mashine hizo zimeweza kutengenezwa na Watalaam wetu kutoka VETA zitaokoa shilingi milioni 14 kwa kila mashine”. Amesema Prof Makubi.

Awali akitoa maelezo juu ya programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema Madini joto ni moja ya kirutubisho muhimu kwa ukuaji mzuri wa akili na mwili wa binadamu na endapo mtu atakuwa na upungufu wa madini joto basi anaweza kupata madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na udumavu wa akili na mwili.

Dkt. Germana amesema katika kukabiliana tatizo la upungufu wa madini joto Taasisi ya Chakula na Lishe inatekeleza programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini kwa kutumia mkakati endelevu wa kuongeza madini joto kwenye chumvi (Universal Salt Iodation) kuanzia miaka ya tisini na mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa angalau asilimia tisini (90%) ya kaya zote nchini zinatumia chumvi yenye madini joto ya kutosha kama inavyopendekezwa na shirika la afya duniani (WHO).

“Serikali kwa kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe kwa kushirikiana na wadau wengine tumefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu na mafunzo kwa wazalishaji chumvi kuhusu uzalishaji bora na uchanganyaji wa chumvi na madini joto, kuhakikisha upatikanaji wa madini joto, kutoa vifaa vya kupimia uwepo wa madini joto kwenye chumvi (Test Kits) na vile vya kuangalia kiwango cha madini joto yaliyomo kwenye chumvi (WYD mashines)". Amesema Dkt. Germana.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Nutrition International Dkt. Daniel Nyagawa amesema katika Mpango mkakati wake wa miaka 6 ulioanza mwaka 2018 hadi 2024 shirika hilo limejielekeza kufanya kazi zake kwa karibu na Serikali na Taasisi zake ili kwa pamoja kuweza kupambana na utapiamlo na madhara yatokanayo na utapiamlo.

Dkt. Nyagawa amesema kwa sasa wanafarijika kuona sasa Mashine hizi zitaweza kupatikana nchini tena chini ya Taasisi ya Serikali hivyo zoezi la ugawaji wa mashine hizi utakuwa endelevu wakati wowote zikihitajika na kuna uwezekano Tanzania ikavuka asilimia 61 ya kaya zinazotumia chumvi yenye madini joto toshelevu endapo zitatumika kikamilifu.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe ameipongeza VETA kwa kuanza kutengeza mashine hizo kwa gharama nafuu tofauti na zingeagizwa toka nje ya nchi na amewaagiza makatibu tawala wa mikoa itakayopewa mashine hizo kuhakikisha wanazitumia ipasavyo na siyo kwenda na kuzifungia stoo.

Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroly Nombo amesema kutengenezwa kwa mashine hizo na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) imejidhihisha kuwa sasa wahitimu na wanafunzi wa vyuo hivyo vilivyopo nchi nzima sasa wameanza kutatua changamoto zinazoikabili jamii na wanaweza kutengeneza vitu amavyo vitapatikana kwa gharama nafuu na kuokoa gharama za fedha za serikali endapo bidhaa hizo zitaagizwa nje ya nchi.







Share To:

Post A Comment: