Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa malipo ya maegesho kwa njia ya Kielektroniki (TeRMIS) unaotarajiwa kuanza kutumika tarehe 1 Machi, 2022 katika Mkoa wa Morogoro.


Akifungua mafunzo hayo Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Meshack Swai ameeleza kuwa TeRMIS ni mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na maegesho ya Vyombo vya Moto (Parking Fee), matumizi ya Hifadhi za barabara (Road Reserve User Charges) pamoja na Adhabu kutokana na Ukiukwaji wa matumizi ya Hifadhi za Barabara.


Amefafanua kuwa mfumo huo ni rahisi, rafiki na salama na utadhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali kwani umeunganishwa na mfumo wa GePG (malipo yanafanyika kwa kutumia “Control number”) ambapo mtumiaji wa maegesho atalipa mwenyewe kwa kutumia simu ya mkononi, Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala wa huduma za Fedha.


Ameongeza kuwa mtumiaji wa maegesho hatalipia maegesho muda huo huo bali atalipia maegesho ndani ya Siku 14 baada ya kutumia maegesho na kwa Mkoa wa Morogoro 

wenye magari watalipa Shilingi 300 kwa saa na Shilingi 1,000 kwa Siku, Pikipiki yenye magurudumu mawili (Bodaboda) Shilingi 300 kwa Siku na Pikipiki yenye magurudumu matatu

(Bajaji) Shilingi 500 kwa Siku.


Mhandisi Swai amesisitiza kuwa timu yake itaendelea kutoa elimu juu ya mfumo wa TeRMIS  kwa wananchi wa Mkoa huo ili waweze kuufahamu na kuutumia.

Share To:

Post A Comment: