Na Joel Maduka Geita 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Geita kuwa sehemu ya mfano kwa kuzingatia usafi katika mazingira yanayowazunguka kwa hiari.


Waziri Bashungwa ametoa wito huo leo Januari 29, 2022 wakati akizindua wa Kampeni ya usafi wa mazingira Mkoa wa Geita na kauli mbiu ya "Mwanamke ni chachu ya usafi wa mazingira; Tuungane katika kutunza mji wetu"


"Utaratibu mliouweka kila wiki kufanya usafi mshirikiane na makapuni yanayochimba dhahabu hapa Geita na wadau wengine kuhakikisha tunakuwa na Geita safi inayomelemeta" amesema Bashungwa


Amesema kuna baadhi ya watu wanapanda daladala na mabasi ya kwenda mikoa wakimaliza kunywa soda na biskuti au kitu chochote kilicho kwenye mfuko au chupa wakimaliza kutumia wanatupa dirishani kitu ambacho tunapaswa kubadiika ili kuweka mazingira safi.


Aidha, Waziri  Bashungwa amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Geita Mjini kushirikiana na  na Baraza la madiwani kuweka mikakati ya  kuboresha stendi ya mkoa ili kuwa na stendi bora na ya kisasa inayotambulisha Mkoa wa Geita.


Vilevile, Waziri Bashungwa amewagiza Wakuu wa Mikoa nchi nzima Kuweka utatatibu mzuri kwa kuweka mazingira wezeshi kwa waendeshabbodabada na kuwapa elimu ya usalama barabarani maana wameisaidia Serikali kujitafutia ajira.


Nae, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule ameeleza kuwa wamekubaliana na wananchi kuhakikisha kila mtu anatunza mazingira katika eneo lake ambapo zoezi la kufanya usafi litakuwa endelevu na litafanyika kila Jumamosi ya kila wiki.


Uzinduzi wa Kampeni hiyo ya usafi ni utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri Bashungwa aliyoyatoa kwa Wakuu wa Mikoa  pamoja na Wakuu wa Wilaya zote nchini kuhakikisha wanasimamia suala zima la usafi hususani katika miradi yote ya barabara, masoko na stendi.

Share To:

Post A Comment: