Hivi majuzi tumesikia na wengine kuona kioja kama si kiroja Job Ndugai (mb) na Spika wa bunge la JMT akipinga wazi Jitihada za Mh. Raisi Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya Chama cha Mapinduzi ambazo zimejikita katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kukopa fedha Tsh 1.3 Trilioni kutoka Benki ya Dunia 

 

Umoja wa vijana wa Chama cha mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro katu hatukufurahishwa na viroja vya spika Mh. Ndugai kwa lengo lake la kumkatisha tamaa Mh. Raisi na Mwenyekiti wa Chama chetu kwenye jitihada zake za kuwaletea watanzania maendeleo. Lakini Umoja wa vijana tukakumbuka hekima ya Shaban Robert katika andiko lake la kusadikika alipohimiza na kutia moyo wapenda maendeleo kwa kusema “KAMA WATU WANAOKUSUDIWA KUWA MWENGE KWA WENGINE WANGALIKUWA WAKINGOJEA SHANGWE LA WATU KABLA YA KUANZISHA MAKUSUDI YAO  MAENDELEO KATIKA MAISHA YANGALIADIMIKA”

     Hivyo basi umoja wa vijana(UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro unamtia moyo Mh. Raisi katika jitihada zake za kimaendeleo kwa kumuhimiza kukazana kutekeleza Ilani ya Chama chetu ambayo inaakisi maendeleo ya watu pasina kungojea shangwe za ndugu Job Ndugai.


Ndugu watanzania;

  Umoja wa vijana pamoja na kumuunga mkono kwa dhati Mh. Raisi lakini unatoa Rai kwa Mh. Spika kujiuzuru nafasi yake ya Spika wa Bunge. Msingi wa hoja hii ni undumira kuwili wa spika wetu ambaye hapo awali alipongeza mikopo hii na baadae kupinga vikali. Hapa inaonekana wazi tatizo sio mkopo bali ana lake . Chama chetu tangu TANU na ASP kimemea kwenye bustani ya ukweli  na kanuni za mwana TANU zilituasa kuwa wakweli kwa kusema NITASEMA KWELI DAIMA FITINA KWANGU MWIKO 

    Hivyo basi, Umoja wa vijana mkoa wa Kilimanjaro tumeamua kusema ukweli huu ambao unamtaka Spika Ndugai ajiuzuru mara moja ili kulinda heshima yake na bunge. Waswahili wanasema “MSIBA WA KUJITAKIA HAUNA KILIO” hivyo fitina na unafiki wa Spika Ndugai unamuwajibisha mwenyewe. 


Ndugu watanzania;

   Umoja wa vijana mkoa wa Kilimanjaro tunaamini msingi wa kanuni zetu tuliyoirithi tokea TANU inayosema “NITAJIELIMISHA KWA KADRI YA UWEZO WANGU WOTE NA KUTUMIA ELIMU YANGU KWA FAIDA YA WOTE” 

 Hata hivyo Mwl Nyerere katika andiko lake la TUJISAHIHISHE  amesema kujielimisha maana yake ni kutafuta ukweli wa mambo. Kwa msingi wa hoja hiyo spika wa bunge Ndugai amepuuza kanuni za chama chetu kwa kushindwa kutafuta ukweli wa mambo hasa ujenzi wa madarasa yaliojengwa nchi nzima kwa manufaa ya vijana wa kitanzania, sio kwamba hajui bali fitina na uroho wenye choyo ya madaraka unamsakama.Share To:

Post A Comment: