Na Rhoda Simba, Dodoma


WADAU wa mradi wa mapambano dhidi ya rushwa ujulikanao “Tuungane kutetea Haki   awamu ya pili unaotekelezwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini[TAKUKURU]  kwa kushirikiana na shirika la Konrad  Adenauer Stiftung[KAS] kutoka nchini Ujerumani wamependekeza Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini iangaliwe upya kwa lengo la kusaidia kuwabana Zaidi viongozi ikiwemo kujiuzulu nafasi zao kwani kutaifishwa mali zao pekee haitoshi.


 


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini hapa  mara baada ya kumalizika kikao hicho,Mwenyekiti wa kikao hicho Dkt.Francis    Michael  ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kutaifishwa kwa mali pekee haitoshi hivyo kuna haja kubwa ya kuangalia upya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.


“Utaratibu huu wa kuwataifisha mali zao halafu wanaendelea na shughuli zao kiukweli haijakaa sawa na haitoi hofu kwani mtu anajua nikitaifishwa mali zangu ajira yangu inabaki kuwa pale pale TAKUKURU inabidi ikae itazame upya sheria hii” amesema  Michael


Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU nchini  Neema Mwakalyelye amesema lengo la mradi wa tuungane ni kuwashirikisha wadau ngazi za vijiji na mitaa hadi Taifa namna ya mapambano dhidi ya rushwa huku meneja mradi wa KAS Tanzania Damas Nderumaki akisema matarajio ya sasa ni kufikia mikoa 24 .


“Tumejipanga kusambaza elimu hii mashuleni,misikitini,makanisani, watendaji wa mitaa kuwashirikisha katika vikao vya halmashauri na pia mtaala mashuleni tunaendelea  kujipanga elimu hii ianzie katika shule ya msingi ili watoto wawe na uelewa  kuhusu rushwa”amesema Neema


 


Kwa upande wao baadhi ya wadau wa mradi wa Tuungane akiwemo Naibu Kamishina Mkuu wa Skauti Tanzania Abdallah Sakasa,mbunge wa Mbagala,Abdallah Chaurembo pamoja  Afisa Uchunguzi  TAKUKURU Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Ilandike Julius wamesema kikao hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya rushwa. 

Share To:

Post A Comment: