Na Mary Gwera, Mahakama
MTENDAJI wa Mahakama ya Rufani (T), Bw. Solanus Nyimbi amewashauri Watumishi wa Mahakama Kuu Zanzibar kuzingatia mambo muhimu matatu ambayo ni Ufanisi, Uwazi na Uwajibikaji ili azma ya uboreshaji wa huduma za Mahakama iweze kufanikiwa kwa ufasaha.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu Zanzibar leo tarehe 08 Desemba, 2021 katika Ofisi ya Uboreshaji wa Huduma za Mahakama (JDU) jijini Dar es Salaam, Bw. Nyimbi ambaye alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa ili kubadili mtazamo na fikra hasi za watu dhidi ya Mhimili wa Mahakama ni vyema kwanza kutengeneza mazingira mazuri ya kutolea haki.
“Nyote mnafahamu kuwa Mahakama ya Tanzania, ipo katika marekebisho/uboreshaji mkubwa ya miundombinu na uendeshaji, yote ikiwa ni katika azma ya kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wateja wanaofika mahakamani. Pia dhamira yetu ni kujenga Imani zaidi kwa wananchi, kuhakikisha ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama na kutoa haki kwa haraka na wakati,” alisema Mtendaji huyo.
Bw. Nyimbi aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha kuhitimisha ziara ya Watumishi wa Mahakama Kuu Zanzibar katika Vituo vya Mahakama Jumuishi, Tanzania.
Mtendaji huyo aliongeza kwa kutoa rai kwa Watumishi hao kuyafanyia kazi mazuri yote waliojifunza katika kipindi cha ziara yao na kuwaomba kuweka bayana yale yote mazuri waliyoyaona kwa kueleza kitu gani kiboreshwe zaidi ili kuboresha hali ya utendaji kazi na utoaji wa huduma katika Mahakama nchini.
“Ninayo imani kubwa kwamba, yote mliyojionea na kujifunza mtayawasilisha kwa viongozi wenu wa Mahakama Zanzibar ili kuendelezea mazuri mliyojionea lakini mabaya mliyojionea myaache huku huku ila yawafundishe kule kwenu msiyafanye,” alieleza Bw. Nyimbi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama (JDU), Mhe. Sekela Mwaiseje alisema kuwa katika kipindi cha ziara yao, Watumishi hao walipata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya Uendeshaji wa Vituo Jumuishi katika Vituo vya Kinondoni na Temeke ambapo kupitia mafunzo hayo walijifunza historia ya uboreshaji wa huduma za Mahakama, maadili, uendeshaji wa Vituo Jumuishi, usimamizi wa mashauri kwa kutumia mfumo wa kuratibu mashauri kwa njia ya Kielektroniki (JSDS II), matumizi ya TEHAMA na Uongozi.
Akiwasilisha taarifa ya ziara ya Mahakama Kuu Zanzibar, mmoja wa Watumishi hao ambaye ni Afisa Takwimu, Bw. Abdulrahman Makame alisema kuwa wamejifunza mambo mengi kupitia ziara hiyo ikiwa ni pamoja na huduma nzuri kwa wateja ‘customer care’, matumizi ya TEHAMA, Utunzaji bora wa kumbukumbu, ufanyaji kazi katika vituo jumuishi.
Mnamo tarehe 07, Novemba 2021 Mahakama ya Tanzania ilipokea ujumbe wa Watumishi 20 wa Mahakama ya Tanzania Zanzibar wa kada mbalimbali wakiongozwa na Mhe. Valentina Katema, Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Zanzibar, lengo la ujumbe huo lilikuwa ni kujifunza namna bora ya uendeshaji wa Vituo Jumuishi vilivyoanza kutoa huduma hivi karibuni.
Post A Comment: