TAASISI ya Maryprisca Woman Empowerment Foundation(MWEF) inatarajia kujenga Hosteli kwa ajili ya watoto wa kike kata ya Mawindi Wilayani Mbarali mkoani Mbeya ili kutatua changamoto za elimu wanazokumbana nazo watoto wa kike wilayani humo.


Hayo yamejiri Disemba 17,2021 wakati wa makabidhiano ya gari aina ya Noah na Pikipiki 4 zenye thamani ya jumla ya Tshs Mil 26.5 zilizotolewa na Diwani wa kata ya Mawindi Sadick Kimelenyi kusaidia huduma za Afya mbele ya Mkurugenzi wa MWEF Mhandisi Maryprisca Mahundi.


Akizungumza,Mhandisi Maryprisca Mahundi ambaye ni Naibu Waziri wa Maji na Mbunge anayewakilisha Wanawake mkoa wa Mbeya amesema ameguswa na hamasa ya kuchangia maendeleo ya jamii iliyofanywa na Diwani Kimelenyi.


"Nampongeza sana Mheshimiwa Diwani,amefanya jambo kubwa la kipekee,linalopaswa kuigwa kwa kuokoa uhai wa wananchi,nitazifikisha taarifa hizi kwa Waziri wa Afya"amesema Mhandisi Maryprisca.


Mhandisi Maryprisca amesema,kwa upande wake ataunga mkono jitihada hizi za kusaidia maendeleo ya kata hiyo kwa kujenga Hosteli ya watoto wa kike katika mwaka ujao wa fedha.


"Kupitia Taasisi ya Maryprisca Woman Empowerment Foundation,tutajenga Hosteli moja kwa ajili ya watoto wa kike na Mwenyezi Mungu atakapotujaalia kwa kushirikiana na Diwani tutaangalia namna ya kupata Hosteli kwa ajili ya watoto wa kiume," amesema.


Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mawindi Sadick Kimelenyi amesema ametoa vyombo hivyo vya usafiri kusaidia huduma kwa wakazi wa sehemu mbalimbali kutoka ndani na nje ya kata ya Mawindi na Wilaya ya Mbarali.


Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mbarali Missana Kwangura amempongeza Diwani wa kata hiyo na kusema kuwa msaada huo utarahisisha huduma katika kituo cha Afya na zahanati zilizopo kwenye kata hiyo.


Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbarali na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wameshukuru Diwani kwa kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020.

Share To:

Post A Comment: