Watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni wapenzi wamekutwa wamefariki huku chanzo kikidaiwa kuwa walikunywa sumu katika Kitongoji cha Mlandizi kata ya Mlandizi Tarafa ya Mlandizi Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, mkoani Pwani.

Akizungumzia tukio hilo la kustaajabisha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema; “Mnamo Tarehe 5 Septemba, 2021 asubuhi huko Mlandizi, watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wapenzi walikutwa wamefariki katika makazi yao baada ya kunywa kitu kinachodhaniwa ni sumu.

“Watu hao ni Godfrey Pius Mandai (48) ambaye alikuwa ni Dereva wa Kampuni na Veronica Gerald (42), mfanyabiashara na mkazi wa Mtwara ambaye alisafiri kutoka Mtwara na kumfuata mpenzi wake huyo Mlandizi.

“Imedaiwa kuwa mwanaume yule alitengengeza juisi ambayo ndani yake ilikuwa na sumu akampa Veronica akanywa na kufariki dunia, mwanaume hutyo alipoona mpenzi wake amefariki na yeye akanywa ile juisi yenye sumu na akafariki dunia.

“Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hili ni wivu wa mapenzi ambapo mwanaume alikuwa akimtuhumu Veronica kuwa anafanya usaliti.

“Kwenye eneo la tukio tumekuta chupa yenye masalia ya sumu na tumekuta pia karatasi ambayo inadhaniwa imeandikwa na mmoja wao ikiwa na maneno yanayosomeka ‘HUU NI USALITI TU.’

 Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi kutokana na tukio hilo,” amesema Kamanda Nyigesa.
Share To:

Post A Comment: