
Picha haihusiani na habari hapa chini
Na Kadama Malunde
Mfanyakazi
wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Debora Rwekwama (34) mkazi wa
Bushushu Mjini Shinyanga amefanyiwa ukatili kwa kushambuliwa kwa kupigwa
sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kukatwa mkono wa kushoto kwa
kisu na mme wake aitwaye Jacobo Mwajenga (35) kutokana na kile
kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio hilo
limetokea Septemba 9,2021 usiku katika mtaa wa Bushushu, Manispaa ya
Shinyanga.
“Usiku
wa Septemba 9,2021 Mfanyakazi wa Benki ya CRDB Debora Rwekwama (34)
(Banker - CRDB) mkazi wa Bushushu Manispaa ya Shinyanga alishambuliwa
kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na baada ya kupoteza fahamu
alikatwa mkono wa kushoto kwa kisu na mme wake aitwaye Jacobo Mwajenga
(35)mkazi wa Bushushu”,amesema Kamanda Kyando.
"Huyu
Jacob Mwajega inasemekana siku ya tukio mchana alienda pale Benki ya
CRDB Mjini Shinyanga akakuta mke wake hayupo pale Benki isipokuwa Hand
bag (Mkoba) wake upo, huyu bwana akamsubiri mkewe, akiwa pale ukataka
kutokea mzozo kidogo pale lakini watu wakaingilia kati kwamba haya mambo
hayafai sehemu za kazi mtaenda kuyaongea huko nyumbani kwenu",ameeleza
"Kwa
hiyo usiku huo huyu bwana Jacobo Mwajenga akamshambulia huyo mke wake
na kusababisha azimie na kumkata jeraha kubwa kweli kweli kwenye mkono
wake wa kushoto na kusababisha mama huyu kuvuja damu nyingi",ameongeza
Baada
ya kufanya tukio hilo, Bushushu Mjini Shinyanga Jacobo Mwajenga
akambeba mke wake akiwa amezimia na kumpakia kwenye gari yao na
kumpeleka hadi katika kituo cha Polisi Kahama.
"Alipofika
katika kituo cha polisi Kahama akaripoti kwamba huyu mama amepata
ajali, kutokana na hali aliyokuwa nayo mama huyo polisi hawakumhoji
kwani alikuwa amezimia walichokifanya ni kumpa PF3 ili huyo bwana
amkimbize mwanamke huyo hospitali na hawakujua kama ni mme wake",amesema.
"Huyu
bwana akampeleka mama huyu hospitali ya wilaya ya Kahama. Sasa
madaktari walivyokuwa wanamchunguza mama huyu hawakuona dalili ya ajali
wakabaini kuwa mama ameshambuliwa wakatoa taarifa polisi na Polisi
tukamkamata huyu bwana Jacobo akiwa hapo hospitali",amesema Kamanda Kyando.
Amesema chanzo cha tukio ni wivu wa mapenzi na kwamba tayari Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa wa tukio hilo.
"Chanzo
cha tukio hili ni wivu wa mapenzi. Huyu bwana yeye ni anafanya kazi ya
Kuongoza watalii kule Arusha. Na kutokana na hii changamoto ya ugonjwa
wa Corona inaonekana kazi yake imepata shida, muda mrefu yupo hapa
Shinyanga anaishi na mke wake, hajishughulishi na kazi yoyote. Mama ni
mfanyakazi wa Benki yeye yupo tu nyumbani,kwa hiyo nafikiri akajenga
tabia ya wivu, na tumebaini chanzo cha tukio hili ni wivu wa mapenzi", ameeleza Kamanda Kyando.
Ameeleza kuwa hali ya majeruhi ni mbaya na amelazwa katika hospitali ya wilaya Kahama.
Kamanda
Kyando amesema hivi sasa kuna matukio mengi ya vifo vinavyotokana na
wivu wa mapenzi hivyo kutoa wito kwamba ukigundua kuwa mwenzako siyo
mwaminifu kwenye mapenzi usijichukulie sheria mkononi,nenda kwa viongozi
wa dini,serikali au vyombo vya dola kuliko kuchukua sheria mkononi
kwani ni kosa la jinai na matokeo yake kuishia jela.
Post A Comment: