-TaSUBa  sasa kurusha vipindi vyake vya elimu ya Sanaa TBC


Na Mwandishi Wetu, Dodoma.


TAASISI ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), imeingia makubaliano ya mashirikiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ili kukuza, kuboresha na kutangaza Sanaa na Utamaduni wa mtanzania kupitia chaneli zake za TBC1,TBC2 pomoja na mitandao ya Kijamii.


Hafla ya utiaji saini huo imefanyika Dodoma katika ofisi za TBC mapema 19 Juni, 2021 baina ya Wakuu wa Taasisi hizo mbili, Dkt. Hebert Makoye kwa upande wa TaSUBa na Dkt. Ayoub Rioba kwa upande wa TBC. 


Awali Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Dkt. Herbert Makoye amesema kama Taasisi wanayo furaha kusaini makubaliano hayo na TBC ambayo ni chombo kikubwa cha habari nchini ikiwemo suala la kutengeneza maudhui hasa eneo ambalo TaSUBa inashughulika nalo kama Taasisi ya mafunzo lakini pia kama Taasisi ambayo inajukumu la kuelimisha umma kwa kutumia Sanaa.


Kutengeneza vipindi vya runinga  kwa njia ya tamthilia ambalo ni jambo la muhimu sana kwa sababu ni njia nzuri ya kuweza kufikisha ujumbe wowote lakini pia ni njia nzuri ya kutangaza lugha yetu ya Kiswahili na Utamaduni wetu wa mtanzania.


Ambapo amebainisha kuwa, itasaidia TaSUBa kuonyesha kazi zinazofanywa kama Taasisi ya mafunzo na itaonyesha mchango wa TaSUBa kwa taifa katika Utamaduni.


"TaSUBa ina malengo pia kusaidia Utamaduni mtanzania uvuke mipaka kwa kutumia vyombo vya habari vyenye nguvu kama televisheni ya taifa (TBC) ili tuweze kufika kwa wenzetu wasije wakafikiri sisi ni wa kupokea tu tamaduni zingine.


"Pia makubaliano haya yatawapa nafasi wanachuo wetu ya kuwa wanafanya mazoezi kwa vitendo kama watatokea wenye uhitaji huo". alisema Dkt. Makoye. 


Kwa upande wake Dkt. Rioba alimshukuru Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kwa hatua waliyofikia ya kusaini makubaliano hayo. 


Amesema Taasisi zote mbili ni Taasisi ambazo zinashughulika na maliasili ya Utamaduni wa mtanzania. 


"Sisi dhima yetu kubwa kama TBC ni kuhakikisha kwamba tunaendeleza na kudumisha Utamaduni kwa sababu utamaduni kama alivyowahi kusema baba wa taifa ni vyenzo muhimu sana katika kumuendeleza binadamu, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na lililokufa". Alisema Dkt. Rioba.


Dkt. Rioba alisema anatambua mchango wa TaSUBa na wanafanya kazi muhimu sana ya kuwaendeleza vijana na imeshakua Taasisi ambayo inatambulika duniani kwa ubora wa kipekee kwa kazi inayoifanya ya kuandaa vipaji kwa ajili ya kukuza na kuendeleza Utamaduni. 


Dkt. Rioba alisisitiz; "Baada ya kusaini makubaliano haya kazi ya kuanza kuandaa kazi za Sanaa itaanza mara moja ili ziweze kuanza kuruka katika vyombo vyetu ambavyo ni redio, televisheni ambayo inaweza ikawa ni TBC1, TBC 2 na mitandao ya kijamii". Alisema.


Aidha Dkt. Rioba aliongeza kuwa anaamini nia waliyonayo TaSUBa na TBC ni ya dhati na wote tunapenda kuona tunaendeleza Utamaduni wetu.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: