Meneja wa Utafiti na Mafunzo Bw. Hamisi Sudi Mwanasala akizungumza na washiriki wa mafunzo kwa wadau wa bidhaa ya mchele yaliyofanyika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Afisa tawala wa wilaya ya Sengerema Bw.Allan Augustine Mhina akifungua mafunzo kwa wadau wa mchele wa wilayani Sengerema mkoani Mwanza .


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji, uchakataji, ufungashaji na uuzaji wa mchele kulipa uzito suala la viwango, ubora na usalama wa bidhaa ili kuweza kuongeza tija.

Wito huo ulitolewa juzi (Ijumaa) na Meneja Mafunzo na Utafiti wa TBS, Hamisi Sudi Mwanasala, wakati akifungua mafunzo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na usindikaji, uchakataji, ufungashaji na uuzaji wa mchele katika Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Yusuf Ngenya.

Mafunzo hayo yaliyoanza Aprili 27, mwaka huu yamefanyika katika wilaya nne kwa nyakati tofauti za Kahama, Bukombe, Katoro, wilayani Geita na kuhitimishwa Sengerema. Mafunzo hayo yametolewa kwa washiriki zaidi ya 300 katika wilaya hizo.

Katika mafunzo hayo washiriki walipewa elimu kuhusu TBS na majukumu yake, kanuni bora za uzalishaji, matakwa ya viwango, namna bora ya uhifadhi, ufungashaji na teknolojia ya vifungashio na taarifa za msingi kwenye vifungashio.

Aidha, Sudi alisema washiriki hao walielimishwa juu ya taratibu za usajili wa bidhaa za vyakula, vipodozi na majengo, kazi ambazo hapo awali zilikuwa zikifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Kwa mujibu wa Sudi, Shirika hilo limeandaa mafunzo hayo ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kikao kilichofanyika Sirari,mkoani Mara, ambacho kiliridhia TBS,itoe mafunzo kwa wajasiriamali wanaosindika, kuzalisha, kufungasha na kuuza mchele katika kanda nzima ya Ziwa.

Alisema wametiwa moyo na mwitikio na ushirikiano mzuri walioupata katika Wilaya zote Kahama,bukombe,Sengerema na mji mdogo Katoro Geita wakati wa maandalizi ya mafunzo haya.

Alisisitiza kwamba mafunzo hayo ni uthibitisho wa azma ya Serikali katika kufanikisha malengo ya Tanzania viwanda.

"Na kwa sababu hiyo tuliona muelekeo mzuri wa usimamizi wa Serikali ya awamu ya tano ambao umeweza kututoa katika uchumi wa chini na sasa tumeingia uchumi wa ngazi ya kati na Awamu ya Sita Kazi inaendelea," alisema.

Alitoa wito kwa watakaoupata mafunzo hayo waweze kuyatumia watakaporejea kwenye shughuli zao. Aliahidi kuwa TBS itaendelea kutoa mafunzo ya namna hiyo kwa wazalishaji, wauzaji na wadau wote wa mchele.

Wakizungumzia mafunzo hayo, washiriki waliipongeza TBS kwa kutoa mafunzo hayo hasa kwa kuzingatia kwamba yametolewa wakati muafaka wa mavuno ya mpunga. Wametoa wito kwa shirika hilo kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: