Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na wanakijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa ufadhili wa Climateworks Foundation na kuipongeza WWF kwa kuyafanyia kazi maono ya serikali ya kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa yakiharibika kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi ikiwemo barafu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipeana mkono na Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru mara baada ya Dkt. Ngusaru kuzungumzia mradi wa miaka miwili wa WWF katika kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, uliowezesha kupatikana Tani 91,000 za samaki aina ya pweza zenye thamani ya Shilingi Milioni 458, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kijijini hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei akizungumza na wanakijiji cha Songosongo (hawapo pichani) kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa ufadhili wa Climateworks Foundation na kuwaasa wanakijiji hao kuhakikisha uvunaji wa samaki aina ya pweza unakuwa endelevu na kutumia vyema kituo hicho ili kiwe na tija katika kuzuia upotevu wa mazao ya uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akimshuhudia Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Kijiji cha Songosongo katika utiaji saini wa makabidhiano ya kituo cha kuzalisha barafu kilichopo Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo hicho.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwasha moja ya mitambo ya kuzalisha barafu ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kutumika kwa kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa ufadhili wa Climateworks Foundation katika Kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo hicho.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiangalia ubora wa barafu iliyozalishwa na moja ya mitambo iliyopo kwenye kituo cha kuzalisha barafu katika kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Amani Ngusaru ambapo kituo hicho kimejengwa na WWF kwa ufadhili wa Climateworks Foundation.

Muonekano wa kituo cha kuzalisha barafu kilichopo Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, kilichojengwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa ufadhili wa Climateworks Foundation kwa thamani ya Shilingi Milioni 424 na kina uwezo wa kuzalisha barafu Tani 1.4 kwa saa 24.

..............................................................................................

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ameupongeza Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa kuyafanyia kazi maono ya serikali ya kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa yakiharibika kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi.
Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (01.05.2021) akiwa katika Kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na WWF kwa ufadhili wa Climateworks Foundation chenye thamani ya Shilingi Milioni 424, kwa ajili ya kuhifadhia samaki wanaovuliwa na wanakijiji hao.
Amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2021/22 imeweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha inaongeza vituo vya kuhifadhia mazao ya uvuvi ili wavuvi waondokane na changamoto ya samaki kuharibika kutokana na ukosefu wa barafu na maeneo ya kuyahifadhia mazao hayo.
“Hali duni inachangiwa na upotevu wa mazao wanayovua kutokana na uvuvi na pia kutokuwa na uhakika wa masoko ya mazao wanayoyapata ndiyo maana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inakuja na suluhu kuokoa wavuvi na watanzania kwa ujumla wake.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha, katika kuhakikisha mazao ya uvuvi yanakuwa na masoko ya uhakika Mhe. Ulega amesema azma ya wizara hiyo ni kuona mazao hayo yanasimamiwa na ushirika hali ambayo itasaidia kuwa na umoja ambao utawezesha wavuvi kusikilizwa na kupata masoko kwa pamoja.
Pia, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi itakuja na mkakati wa usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya vichanja maalum kwa ajili ya kukaushia dagaa na samaki ili kuzuia mazao hayo kutokuwa na mchanga na kuyaongezea thamani kwa kupata masoko zaidi ndani na nje ya nchi hali itakayobadilisha uchumi wa wavuvi na serikali kupata mapato zaidi.
Kuhusu zao la mwani ambalo wanakijiji cha Songosongo wamelalamikia kukosa masoko hali inayosababisha nyumba zao kurundikana zao hilo na hatimaye kuharibika na wakati mwingine kuuza kwa bei ndogo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema katika kipindi hiki wizara itapitia upya sheria inayosimamia zao la mwani ili kubaini changamoto ambazo ni kero kwa wafanyabiashara wa zao hilo na kuziondoa ili wakulima wa mwani na wafanyabiashara waweze kunufaika.
“Moja ya jambo ambalo pamoja na kutafuta soko la mwani tutengeneze kiwanda kidogo cha kukausha mwani na kuliongezea thamani zao hilo ili wakulima waweze kuhifadhi vizuri mwani na kuuza kwa bei nzuri zaidi kuelekea katika uchumi wa bluu.” Amefafanua Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa kupitia zao la mwani wanakijiji cha Songosongo wataweza kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na mwani ikiwemo sabuni na kuuomba Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kufikisha elimu ya ujasiriamali kwa wanakijiji hao juu ya masuala ya ujasiriamali.
Naibu Waziri Ulega pia amesema ni wakati muafaka kwa serikali kuangalia upya Vikundi vya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) badala ya kulinda rasilimali za uvuvi pekee viweze kunufaika kwa kupata mikopo na kuendesha shughuli zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania Dkt. Amani Ngusaru amesema kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa katika Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi chini ya ufadhili wa Climateworks Foundation chenye thamani ya Shilingi Milioni 424, kina uwezo wa kuzalisha barafu Tani 1.4 kwa saa 24.
Dkt. Ngusaru amesema mradi huo umeenda sambamba na uhamasishaji wa ufungaji wa miamba ya samaki aina ya pweza ambapo inakadiriwa kwa kipindi cha miaka mwili ya mradi, Tani 91,000 za pweza zimevuliwa katika Kijiji cha Songosongo zenye thamani ya Shilingi Milioni 458, ambapo fedha hizo zimetokana na ufungaji wa miamba kwa awamu tano.
Ameongeza kuwa kuhusu changamoto za zao la mwani anaanza kulifanyia kazi kwa kuwasiliana na makao makuu ya WWF ili kupata namna bora ya wakulima wa zao la mwani hapa nchini wakiwemo wa Kijiji cha Songosongo kuwa na masoko ya uhakika ya zao hilo.
Aidha, kuhusu kilio cha kukosekana kwa boti ya doria kwa ajili kikundi cha BMU katika Kijiji cha Songosongo, Dkt. Ngusaru amesema WWF imepokea kilio hicho na kuahidi kuleta boti na injini yake ili kurahisisha shughuli za doria katika maeneo ya miamba ya uzalishaji wa samaki aina ya Pweza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei amesema ili kuhakikisha kituo cha uzalishaji barafu kilichopo katika Kijiji cha Songosongo kinakuwa na tija ni lazima uvuaji wa samaki aina ya pweza uwe endelevu na kuhakikisha upotevu wa samaki hao unapunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Dkt. Kimirei ametolea mfano wa moja ya mitambo ya uzalishaji barafu iliyowekwa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika lakini wavuvi wakafikiri barafu zinaharibu samaki na hawakutaka kuutumia, lakini wavuvi hao walipokuja kugundua faida ya barafu hivi sasa mahitaji ya barafu hayatoshi.
Amefafanua kuwa mitambo hiyo ni muhimu na imetumia fedha nyingi hivyo wanakijiji cha Songosongo waweze kutumia kwa namna ambavyo imepangwa kutumiwa na kuitunza mitambo hiyo kwa ajili ya uhifadhi wa samaki aina ya pweza pamoja na samaki wengine.
Nao baadhi ya wanakijiji cha Songosongo wamesema wamefurahishwa na kuwepo kwa kituo hicho cha kuzalisha barafu hali ambayo itawasaidia kuzalisha barafu kwa wingi na kutunza samaki ili wasiharibike na kuiomba serikali pamoja na WWF kuangalia namna ya kuwasaidia waweze kunufaika na zao la mwani kwa kuwa kwa sasa wafanyabiashara wengi wanashindwa kwenda kununua kutokana na gharama za ushuru hali inayosababisha wakulima wa zao hilo kufikia kuuza Kilogramu Moja ya mwani kwa Shilingi 400.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: