Na Elizabeth Joseph,Arusha.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella ameahidi kushughulikia suala la usafi Jiji la Arusha kwa kukaa meza moja na wananchi bila kutumia nguvu.


Amesema hayo leo mkoani humo wakati wa kikao utambulisho na viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini,mashirika ya Serikali,watendaji na wafanyabiashara wa Mkoa huo.


Ameeleza kuwa Serikali na  wananchi kwa pamoja wakiwa na nia ya dhati ya kuisukuma Arusha mbele watafanikiwa katika suala hilo.


"Agenda yetu iwe ya kuisukuma Arusha kusonga mbele,hakuna haja ya kutumia ubavu tutaelewana tu,wale ni wananchi wetu tutakaa meza moja tujadili hili la usafi"Alisema Mongella.


Ameongeza kwa kuwaahidi wananchi wa Mkoa wa Arusha kuongoza Mkoa huo kwa uongozi shirikishi hivyo kuwaomba yeyote mwenye wazo la maendeleo ya Arusha Ofisi yake iko tayari kulipokea na kulijadili pamoja.


Kuhusu utalii Mongella amesema watahakikisha juhudu zinatolewa katika kufanikisha na kukuza utalii mkoani humo licha ya kuwepo kwa changamoto ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona.


Awali akitoa salamu pamoja na kuaga rasmi viongozi hao,Mkuu wa Mkia mstaafu Idd Kimanta alimuomba Mkuu huyo kuhakikisha anakamilisha utekelezaji wa hospitali za Wilaya ya Longido,Ngorongoro pamoja na ujenzi wa Ofisi ya kisasa ya Jiji la Arusha.


"Jiji la Arusha halina Ofisi mafaili ya Jiji yanatembezwa kutoka Jiji kupelekwa Njiro,kutoka Jiji kupelekwa Kilombero nilitamani kuona jengo kubwa jiji lenye hadhi ya Geneva of Afrika............


"Kitu kingine ambacho nilitamani kukiona ni usafi wa Jiji la Arusha,tuna tofauti gani na Moshi?,nilitamani kukiona Geneva of Afrika lakini naamini utaitengeneza,nilikuwa nasubiri kusimamishwa kazi kwaajili ya usafi Mheshimiwa Dc anajua hili, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa vaa uso wa chuma,ziba masikio safisha Jiji,zitapigwa simu,utasemwa sana achana na maneno safisha Jiji"Alisisitiza Kimanta.


Kimanta pia alitaja changamoto nyingine ni kuporomoka kwa utalii na kusema kwasasa magari ya kubeba watalii yamegeuka kubeba Arusi jambo ambalo kiliniumiza sana katika kipindi chake cha uongozi.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: