Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuanza rasmi kwa utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme kupitia miradi ya PERI URBAN na DENSIFICATION  yenye jumla ya gharama ya Tsh 68 bilioni,ambayo itayafikia maeneo zaidi ya 120 katika Kata na Mitaa ya Dodoma Jiji ambayo haikuwa na nishati ya umeme.


Mavunde ametoa shukrani hizo leo wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Mh. Dr. Medrad Kalemani katika mitaa ya Chimala na Bwawani kata ya Ntyuka kukagua utekelezaji wa mradi huo wa usambazaji umeme katika Kata na mitaa yote ya Jimbo la Dodoma Mjini,ambapo Waziri Kalemani amewata wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha kazi ya usambazaji wa umeme katika maeneo yote ya Jiji la Dodoma ndani ya muda ulioanishwa kwenye mkataba ili ndani ya miezi 12 maeneo yote 120 yawe yamepata umeme.


“Leo nimekuja kukagua mwenyewe zoezi la usambazaji umeme hapa Jijini Dodoma na niwaondoe hofu wananchi wa Dodoma Jiji ambao bado kuna changamoto ya nishati ya umeme kwamba ndani ya miezi 12 Dodoma yote itawaka kupitia utekelezaji wa miradi hii mikubwa,nichukue pia fursa hii kuwataka REA na TANESCO kuhakikisha kwamba wananchi wote wa maeneo haya ya pembezoni wanaunganishia umeme kupitia miradi hii kwa gharama ya Tsh 27,000 na si vinginevyo”Alisema Dr.Kalemani


Wakati huo huo,Waziri Kalemani ametumia fursa hii kuwahakikishia watanzania juu ya utatuzi wa changamoto ya kukatika katika kwa umeme na kwamba jambo hilo halitatokea kwasababu ya ukarabati wa mitambo uliofanyika,na pia amewakumbusha Mameneja wote wa TANESCO ambao watakuwa wameshindwa kuwaunganishia umeme wananchi kuachia ngazi baada ya tarehe 15.04.2021 kufuatia agizo lake alilolitoa miezi mitatu kabla.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: