Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo, akitoa salamu za Shirika lake mbele ya wajumbe wa mkutano huo wa Mwaka wa MJUMITA.
IMEELEZWA kuwa Sekta ya Misitu ikisimamiwa vizuri na kwa uendelevu italeta mchango chanya katika sekta zinazotegemea mifumo ikolojia ya Misitu ya asili kama vile Kilimo, Maji,Wanyamapori, na nishati.
Hayo yalisemwa na Nanjita Nzunda Muwakilishi wa KatibuTawala wa Mkoa wa Morogoro kwenye ufunguzi wa Warsha na mkutano Mkuu wa 20 wa mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misiti Tanzania MJUMITA uliofanyika Mkoani Morogoro.
Alisema kuwa sera na sheria ziko wazi na zinawezesha vijiji kuanzisha na kurasimisha misitu yao na kuandaa mipango yao ya usimamizi, sheria ndogondogo na mipango ya uvunaji.
“Kwa kurasimisha Misitu yao ya hifadhi, vijiji vinakuwa na mamlaka ya kusimamia na kunufaika kwa asilimia Mia moja na Misitu huo lakini pia kunatoa fursa kwa Kijiji husika kuusimamia huo Msitu kwa manufaa ya Wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa Misitu” alisema Nzunda.
Aliongeza kuwa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya Jamii ni nyenzo kuu ya uhifadhi wa Misitu kwani wananchi wanakuwa na na mamlaka ya kuusimamia Msitu husika kulingana na Mipango yao ya Usimamizi na sheria ndogo walizojiwekea.
Nzunda alibainisha kuwa pamoja na faida hizo lakini kila Mwaka Tanzania inapoteza hekta zaidi ya 460,000 za Misitu kiasi ambacho ni kikubwa sana hivyo kila Mtanzania anapaswa kuchukua za makusudi kunusuru Misitu.
“ Nawapongeza sana MJUMITA na TFCG kwa kuwezesha vijiji kuanzisha misitu ya hifadhi ya vijiji Kilosa,Mvomero,Morogoro,Kilwa,Lindi, Liwale,Tunduru, Nachingwea, Handeni na Kipindi ambako zaidi ya vijiji 100 vimewezeshwa na nimefurahi kusikia kwamba mashirika haya mawili yamewezesha Misitu ya Hifadhi zaidi ya 50 kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (Gazettment).
Aliongeza kuwa Misitu hiyo ina jumla ya Hekta 168,331.38, na kwamba hayo ni mageuzi makubwa katika sekta ya Misitu na nu Misitu ya mfano kufikia hatua hiyo.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi huyo kufungua warsha na mkutano huo Mkuu Mwenyekiti wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania MJUMITA, Revocatus Njau alisema kuwa MJUMITA ni chombo cha Kitaifa ambacho kinaunganisha Jamii zinazoishi kandokando ya misitu ya asili na kuwa na sauti ya pamoja juu ya usimamizi wa Misitu na utawala Bora.
Mwenyekiti huyo alisema mtandao huo ulianzishwa Mwaka 2000 na ilisajiliwa Kama NGO Mwaka 2017 na mtapa sasa ina mitandao 100 katika Kanda sita za Tanzania na kwamba ina wanachama katika vijiji 452 kwenye mikoa 30 ya Tanzania bara.
“ Kupitia jitihada hizo kubwa za TFCG na MJUMITA zinewwzesha kuboresha maisha ya jamii kupitia shughuli mbalimbali kama vile ufugaji wa Nyuki,Kilimo,Kilimo hifadhi,miradi ya maji,ufugaji vipepeo, uzalishaji wa Mkaa Endelevu na uanzishwaji wa ViCOBA” alibainisha Njau.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa MJUMITA ineweza kuwaleta Pamoja takribani Wanachama 15,000 katika usimamizi wa Misitu ya asili vijijini wakisimamia Misitu zaidi ya hekta 1,800,000 katika vijiji viwili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahma Njaidi alisema kuwa Warsha na Mkutano huo Mkuu wa Mwaka hufanyika kila Mwaka na kuwakutanisha wajumbe kutoka nchi nzima ili kujadili changamoto na mafanikio yanayopatikana kila Mwaka na kuyatafutia ufumbuzi wa pamoja.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa misitu bado inaangamia kutoakana na kazi mbalimbali za kibinadamu hivyo kuna kila sababu ya kurasimisha Misitu hiyo iliyo kwenye vijiji nchi nzima ili kupunguza uharibifu unaofanyika kiholela ili itunzwe na kutumika kwa njia endelevu kwa maslahi ya vijiji na Taifa kwa ujumla.
“ Tukiacha uharibifu huu uendelee tutaifanya nchi yetu kuwa jangwa na sisi hatuwezi kuruhusu Hilo litokee hivyo tuisaidie Serikali maana sisi ndio tupo huku chini tunajua kinachoendelea” alisisitiza, Njaidi.
Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa NAFOMA uliofanyika Mwaka 2017 ulionyesha zaidi ya hekta 4069 inapotea kutokana na uharibifu wa aina mbalimbali za misitu.
“ Ni wajibu wetu wananchi kuhakikisha tunatunza misitu yetu nchi nzima kwa kupanga namna bora ya kusimamia lakini pia mapato yanayopatikana kutokana na mazao ya misitu hiyo yatumike kwenye vijiji kwenye miradi ya maendeleo kama motisha ya usimamizi huo” alisema Lyimo.
Lyimo aliwataka wajumbe wa mkutano huo kutambua kuwa wakati umefika jamii na serikali iwekeze kwenye Misitu ili itangazwe kwenye gazeti la Serikali ili kuvipa vijiji nguvu za kuisimamia vizuri kisheria na kuongeza misitu ya hifadhi ya jamii inayosimamiwa kutoka hekta milioni mbili kwa sasa na kuifikia misitu hekta milioni 22 ambayo haijaifadhiwa kwa sasa.
Mashirika ya MJUMITA na TFCG wanatekeleza Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) chini ya Mradi wa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) na mradi wa kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoFOREAT) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
Post A Comment: