Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Benjamini Sitta akifurahia jambo wakati wa kikao cha Baraza la madiwani robo ya tatu ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Aron Kagurumjuli na Kushoto ni Naibu Meya Mhe. George Manyama.

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni wakiwa kwenye kikao cha robo ya tatu ya baraza hilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Bwana Aron Kagurumjuli akizungumza na madiwani pamoja na watendaji 




Baraza la madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni limempongeza  Mkurugenzi Ndugu. Aron Kagurumjuli kwa kutekeleza miradi mikubwa katika kipindi cha miaka mitano ya utendaji wao wa kazi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mstahiki Meya Mhe. Benjamini Sitta kwa niaba ya  Baraza la madiwani lililofanyika katika ukumbi wa mikutano ya Halmashauri hiyo.

Meya Sitta amesema kuwa katika kipindi ambacho wamekuwa madiwani wameshuhudia miradi mikubwa ambayo imetekelezwa ikiwa ni  juhudi kubwa zilizofanywa na Mkurugenzi Kagurumjuli.

 Ameongeza kuwa Kinondoni imekuwa na mafanikio makubwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya elimu, Afya, Miundombinu, Masoko na Mazingira.

Mbali na miradi hiyo mikubwa, ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Stendi ya Kisasa ya daladala ya mwenge, Ofisi ya kisasa ya Manispaa, uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu,  Soko la kisasa  Magomeni, Tandale ambapo yote inatekelezwa na mapato ya ndani.

“ Miradi iliyotekelezwa ni mingi na wote humu ndani ni mashahidi, hiyo tuliyotaja ni baadhi tu, lakini ukiangalia katika sekta ya elimu na Afya huko nako pia Meya na Mkurugenzi wamefanya kazi kubwa sana ambayo wanastahili pongezi kubwa” amefafanua Mhe. Sitta.

Aidha aliongeza kuwa kwaupande wa fedha za asilimia kumi kwa ajili ya mikopo ya vijana, wazee na walemavu kupitia uongozi huo fedha hizo zimetumika vizuri na kwamba walengwa wamefikiwa na fedha hizo.

Diwani wa Kata ya Wazo, Mhe. Joel Mwakalebela amesema kuwa kata yake pia imenufaika na fedha za  Halmashauri hiyo katika sekta ya elimu na Afya kwani wananchi wake wamepata madarasa ya kisasa pamoja na vituo vya afya kazi kubwa ambayo imefanywa na Mkurugenzi Kagurumjuli.

Mwakalebela  amesema Mnispaa hiyo inaongoza kwa kuwa na barabara nzuri za lami kwa kila mtaa sambamba na mifereji ambayo imeweza kujengwa maeneo mengi yaliyokuwa na changamoto hiyo.

“ Ukipita kwenye mitaa huwezi kuona barabara ambazo hazipitiki, hata mvua ikinyesha ya namna gani, kwa hili kwakweli ninampongeza sana Mkurugenzi na timu yako,halmashauri hii inaviongozi wachapa kazi” amesema Mhe. Mwakalebela.

 Kwaupande wake Mkurugenzi Kagurumjuli ameeleza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo umetokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ofisi yake na Meya pamoja na watendaji kwani kila mmoja amekuwa akitimiza majukumu yake pasipokuwa na migongano.

Amesema ushirikiano huu mkubwa umewezesha Halmashauri hiyo kuwa na maendeleo makubwa kwenye kila nyanja kama vile Elimu msingi na Elimu Sekondari, Afya, Masoko, miundombinu sambamba na mazingira.

“ Tangu tumeingia kwenye utawala huu, nikiwa na Meya Sitta hatujawahi kuwa na migogoro , watendaji wamekuwa na muda mwingi wa kufikiria mambo makubwa ya maendeleo jambo ambalo limetufikisha kwenye mafanikio makubwa nandio mana leo tunapongezana hapa.

Katika hatua nyingine baraza hizo limepitisha taarifa za kamati mbalimbali ambazo ni kamati ya Fedha na uongozi, Huduma za Uchumi, Kamati ya kudhibiti  UKIMWI, Kamati ya Maadili pamoja na kamati ya mipango miji na mazingira.



Imeandaliwa na Kitengo Cha Habari na Uhusiano


Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Share To:

Post A Comment: