Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe amewataka washauri elekezi waliosaini mikataba ya kusanifu miundombinu kwa ajili ya utekelezaji mradi wa kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) kuifanya kazi hiyo kwa weledi na ubora.
Ametoa Rai hiyo jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini mikataba mitatu na Makampuni yenye thamani ya Shilingi Milioni 868.7 ,randama mbili za mashirikiano na taasisi za TBS na VETA kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu nchini ,katibu huyo amesema Serikali haitawavumilia watu wazembe.
“Nawaambieni mfanye kazi zenu kwa weledi maana Wizara ya Kilimo tunazingatia weledi ,hivyo hatutamvumilia mshauri elekezi ambaye ni mzembe ,tutawasimamia kwa karibu na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye miradi hii ya kudhibiti sumukuvu” amesema Mhandisi Mtigumwe.
Aidha ameelezea Kampuni zilizo saini mikataba hiyo kuwa ni M/S Digital Space kusanifu karantine ya maabara ya utafiti wa magonjwa ya kibaiolojia,Sundy Merchant Ltd kufanya tathmini ya awali ya mradi wa Sumukuvu na A.V Consult kufanya usanifu na ujenzi wa maghala 14 ya hifadhi ya Mahindi na Karanga.
Aidha, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini randama ya mashirikiano ya kufundisha vijana mafundi mchundo 400 kutengeneza teknolojia ya kuhifadhi mazao wakati Shirika la Viwango (TBS) limeingia makubaliano na Wizara ya Kilimo kusaidia kutoa elimu kwa wajasiliamali na Wafanyabiashara kuzalisha na kuhifadhi mazao kwa kuepuka sumukuvu ili wapate soko la uhakika na salama katika mnyororo wa thamani ya mazao nchini.
Akizungumza wakati wa utiaji saini Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini Dkt.Pancras Bujulu amesema ni fursa nzuri wamepata kufundisha mafundi mchundo kutengeneza vihenge rahisi kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya wakulima ili kulinda afya za watu kwa kutumia teknolojia bora.
“Ni wajibu wetu VETA kutoa mafunzo kwa vijana Nchini ili wazalishe vifaa bora (Vihenge) kwa ajili ya kuhifadhi nafaka na kujipatia ajira” Dkt.Bujulu amesema
Amefafanua kuwa Vijana hao 400 toka wilaya 18 za Tanzania Bara watakuwa chachu ya kusambaza teknolojia hiyo kirahisi na bora ya uhifadhi nafaka hapa Nchini na kuwafanya na baadhi ya Vijana wengine nao waweze kujifunza kutoka kwao.
Naye mratibu wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu (Tanzania Iniatives for Preventing Aflatoxin Contamination-TANIPAC) Clepin Josephat amesema mradi huo ni wa miaka mitano(2019-2023) unatekelezwa Nchini kwa lengo la kuhakikisha usalama wa chakula hususani kwenye mazao ya Mahindi na Karanga hayachafuliwi na fangasi wanaosababisha sumukuvu.
Ameeleza kuwa sumukuvu inadaiwa tangu ilipogunduliwa Nchini imesababisha madhara kwa Wananchi ikiwemo kuongezeka kwa uwezekano wa kansa ya ini,udumavu kwa watoto chini ya miaka 5 na wengine imewapelekea vifo.
Katika mwaka 2016 jumla ya watu 19 walikufa na wengine 68 waliugua na kulazwa kutokana na sumukuvu aina ya Aflatoxin kwenye mikoa ya Dodoma na Manyara ambayo imeathirika zaidi.
Post A Comment: