Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha Omari Lumato ameongoza vijana wa Wilaya ya Meru kuchangia damu katika hospitali ya Patandi iliyoko halmashauri ya wilaya ya Meru ambapo vijana wengi wamekjitokeza kujitolea damu ili kusaidia majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro hivi karibuni.
Lumato amewapongeza vijana wa chama hicho wilaya ya Meru kwa kuwa mstari wa mbele katika zoezi la utoaji damu ambalo wamelifanya kwa lengo la kusaidia wagonjwa wanaohitaji damu na kunusuru maisha yao.
Aidha ameziomba mamlaka husika kutunza damu hizo na kuwapatia wagojwa bila malipo yoyote ili zoezi hilo liwe na Baraka kwa watoaji wa damu waliojitolea.
Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Meru , Faraja Laizer amesema kuwa mwamko wa vijana katika kujitolea damu umekua mkubwa hivyo wanajipanga kuweka ratiba za zoezi hilo kila baada ya miezi mitatu ili kuokoa maisha ya watu  kwa kuchangia damu.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru ,Dr. Maneno Focus amewapongeza vijana hao wa CCM kwa kuona uhitaji mkubwa wa damu ulioko katika hospitali ya wilaya hiyo pamoja na vituo vya afya vinavyofanya upasuaji vinahitaji  huduma hiyo muhimu.
Mhamasishaji wa Damu salama Wilaya ya Meru Elizabeth Mohere amesema kuwa damu hizo zitatumika kuokoa maisha ya kinamama wajawazito ambao wakati wa kujifungua hupoteza damu nyingi sana hivyo zitanusuru maisha yao.
Pia amewaomba vijana kujenga utamaduni wa kujitolea damu ambao utaokoa maisha ya watu wengi hususani majeruhi wa ajali ambao hufikishwa hospitalini hapo.

Matukio mbalimbali Katika Picha.












Share To:

msumbanews

Post A Comment: