Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, ameipongeza Benki ya UBA Tanzania kwa mchango mkubwa ambao inatoa kwenye sekta ya elimu kwa kutoa vitabu zaidi ya 15,000 kwa shule za sekondari zote zenye uhitaji wa vitabu zilizopo wilaya humo.

UBA Tanzania kupitia UBA Foundation chini ya mpango wa ‘Read Africa Initiative’, imetoa vitabu hivyo vya fasihi kwenye shule za Serikali zilizopo wilaya mpya ya Kigamboni.

Shule ambazo UBA imetembelea ni Nguva Sekondari, Aboud Jumbe Sekondari na Pemba mnazi Sekondari zote zipo ndani ya wilaya hiyo.

Wengine waliokuwepo kwenye tukio hilo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigamboni, Ng’wilabuzu Ludigija na Ofisa Elimu wa Wilaya, ambapo uongozi wa benki hiyo uliongozwa na Geofrey Mtawa ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Biashara ndogondogo na za Kati, Mkuu wa Kitengo cha Dijitali, Asupya Nalingigwa na Ofisa Mawasiliano, Anitha Pallangyo.

“Vitabu hivi vilivyotolewa na Benki ya UBA Tanzania, vitasaidia katika kuwajengea vijana wetu kupenda kujisomea na kujiwekea utaratibu wa kujisomea mara kwa mara, pamoja na kuwaongezea uwezo katika masomo yao,” amesema Msafiri.

Geofrey alisema vitabu hivyo ni vya hadhi ya juu Afrika, ambavyo vimeboreshwa zaidi ili kuwawezesha wanafunzi na walimu kuvielewa kwa lugha rahisi na yenye kuelimisha.

Mbali na kutoa vitabu hivyo, UBA imekuwa ikisaidia sekta ya elimu kwa kutoa vitabu kwenye shule mbalimbali ikiwa ni pamoja na wilaya za Ilala, Temeke nkoani Dar es Salaam na Kisarawe mkoani Pwani, pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali bure kwa vijana na wanawake kupitia mpango wao wa ‘Each one teach one’.
Baadhi ya vitabu vilivyotolewa na benki hiyo ni vile vinavyotumika kwenye mitaala ya Tanzania kama ‘Things Fall Apart’, ‘The Girl That Can’, ‘The Fisherman’ na vinginevyo vingi kutoka kwa waandishi mashuhuri kutoka Nigeria ambavyo pia hutumika kwenye mitaala ya shule mbalimbali Afrika.
Mwisho
Share To:

Post A Comment: