Jeshi
la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
limekusanya Sh972.7 milioni za makosa ya usalama barabarani katika
kipindi cha wiki mbili.
Katika
operesheni hiyo ya ukamataji wa magari iliyofanyika kati ya Mei 11 hadi
Mei 24, mwaka huu magari yaliyokamatwa ni 24,116, pikipiki 763 na
daladala 10,301.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kamanda wa kanda
hiyo, Lazaro Mambosasa alisema, “Waendesha babodada waliofikishwa
mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mishikaki
(abiria zaidi ya mmoja) ni 59. Jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 30,850
na fedha zilizopatikana ni Sh972 milioni.
“Madereva
na wamiliki wa magari wanatakiwa kulipa faini zao ndani ya siku saba
ili kuepuka faini kuongezeka na kusababisha kukamatwa tena kwa
kulimbikiza madeni,” alisema Mambosasa.
Katika
hatua nyingine; Mambosasa alisema polisi wanamshikilia mhudumu wa
Hoteli ya Sleep Inn kwa tuhuma za kukutwa na sare za polisi, silaha,
cheo cha koplo, pingu na nguo inayofanana na sare za Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ).
“Tulipata
taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu mmoja anatumia sare za polisi
kuwakamata watu na kuwafunga pingu na kuwatishia bastola ili kufanikisha
kupora mali maeneo mbalimbali ya Jiji. Baada ya kupata taarifa hizo
tulianza ufuatiliaji na kuweka mtego. Mei 12 tulifanikiwa kumkamata
mtuhumiwa,” alisema Mambosasa.
Post A Comment: