MSANII wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ amehukumiwa kulipa faini ya Tsh. Milioni 14 na mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya utapeli kusababisha hasara kwa kushindwa kufika kwenye shoo.

Katika kesi hiyo iliyotolewa hukumu leo Machi 1, 2018, imethibitika kuwa Shilole  alichukua kiasi cha Tsh. Milioni tatu kwa Mary Musa kwa ajili ya kufanya shoo siku ya mkesha wa Pasaka mwaka jana 2017 katika Ukumbi wa Heinken uliopo Mbagala-Kijichi jijini Dar es Salaam na kushindwa kufika kwa muda waliokubaliana.

Kutokana na kitendo hicho,  mashabiki waliofika kwenye shoo hiyo walifanya vurugu na kumsababishia mwandaaji ambaye ni Mary, hasara ya Tsh. Milioni 14 ambazo mahakama imeamua Shilole azilipe kama fidia kwa mlalamikaji.

Akisoma hukumu hiyo, hakimu wa mahakama ya Mwanzo Kinondoni, A. P. Mshingwa amesema Shilole amekuwa akitumiwa wito mara kwa mara na mahakama afike kusikiliza kesi yake lakini amekuwa akikaidi kufanya hivyo hadi mahakama ilipomuandikia wito mwingine kwenye Gazeti la Uhuru lakini hakufika pia.

Mahakama imemuamuru azilipe pesa hizo haraka ndani ya wiki moja vinginevyo mali zake zitaanza kukamatwa.

Shilole aliambatana mahakamani hapo na mumewe, Ushebe,  na wakili wake ambaye baada ya kufuatwa kwa mahojiano na waandishi wa Habari walikataa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: